Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na kazi kubwa ya kupambana na makundi ya nzige yaliyovamia nchini iliyofanywa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana mashirika mawili ya kupambana na nzige barani Afrika.
Kazi hiyo inafanywa na Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani la Afrika Mashariki (Desert Locust Control Organisation for Eastern Africa-DLCO EA) na Shirika la Kudhibiti Nzige Wekundu la Kusini na Kati mwa Afrika (International Red Locust Control Organisation for Central and Southern Africa-IRLCO CSA).
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Machi 4, 2021) wakati akizungumza na wananchi katika kijiji cha Engaruka, wilayani Monduli mkoani Arusha mara baada ya kukagua shughuli ya udhibiti wa nzige katika kata ya Engaruka.
Amesema ameridhishwa na kazi nzuri ya kupambana na nzige iliyofanyika tangu makundi hayo yalipongia nchini, ambapo amesisitiza licha ya kazi nzuri iliyofanyika ni muhimu kwa Wizara ya Kilimo ikaweka mikakati ya kukabiliana na makundi hayo pindi yatakapoingia tena.
“Lazima tuwateketeze, nzige ni hatari na hawapaswi kupewa nafasi hata ya dakika moja kuingia kwenye mashamba yetu. Nzige hawa wana uwezo wa kusafiri umbali wa kilomita 200 kwa siku na kuteketeza zaidi ya hekta mbili kwa siku, hivyo ni lazima tuwateketeze.” Majaliwa
“Muhimu zaidi ni kujipanga vizuri kukabiliana nao, ni lazima tuendeleze kazi nzuri tuliyoianza. Hawa wadudu ni hatari na wanazaliana mno. Ukimuona, kawaida anakuwa na rangi nyekundu lakini ukimuona ana rangi ya njano huyo amebeba mayai tuwatekeze ili wasizaliane,” Majaliwa
Waziri Mkuu amesema watalaamu wa Tanzania na wataalamu kutoka Zambia, Zimbabwe, Uganda na Kenya wanashirikiana kupambana na nzige kwa kutumia vifaa mbalimbali kama ndege, helikopta na mitambo ya kupulizia kwa mikono.
Amewapongeza wananchi kwa ushirikiano wanaoutoa kwa wataalamu kwa kutoa taarifa pale wanapoona makundi ya nzige na kwenda kuwaonesha wataalamu na amewasihi waendelee kupambana na makundi hayo “Watanzania na Wana-Engaruka tuendelee kutoa taarifa na kujitokeza kwa wingi kushirikiana na wataalamu wetu kuteketeza makundi hayo,”.