“Mgogoro wa njaa unakaribia” kwa raia wa Sudan Kusini wanaorejea nchini mwao baada ya kukimbia mapigano ambayo yamekuwa yakisambaratisha nchi jirani ya Sudan kwa zaidi ya miezi mitano, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) lilionya Jumanne.
Tangu kuzuka kwake Aprili 15, vita nchini Sudan kati ya jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhane na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) cha naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo vimesababisha vifo vya karibu 7,500, kulingana na makadirio ya uchambuzi wa kina wa Mradi wa Data ya Mahali pa Migogoro ya Kivita na Tukio lisilo la Kiserikali.
Pia iliwakosesha makazi zaidi ya watu milioni tano, wakiwemo milioni 2.8 waliokimbia mji mkuu Khartoum, eneo la mashambulizi ya anga, mizinga na mapigano mitaani.
Wengi wa watu waliokimbia mapigano na kuvuka mpaka na kuingia Sudan Kusini ni Wasudan Kusini ambao “wanarejea katika nchi ambayo tayari inakabiliwa na mahitaji ya kibinadamu ambayo hayajawahi kushuhudiwa”, inasisitiza WFP katika taarifa kwa vyombo vya habari.
“Tunaona familia zikihama kutoka janga moja hadi jingine, wakikimbia hatari nchini Sudan na kujikuta wakikabiliwa na kukata tamaa nchini Sudan Kusini,” anasema Mary-Ellen McGroarty, mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Kusini.
Hata hivyo, WFP haina “rasilimali muhimu kutoa msaada muhimu kwa wale wanaouhitaji zaidi,” anaonya.
Raia wa Sudan Kusini “wanavuka mpaka bila chochote ila nguo migongoni mwao”, na wengine pia ni wahanga wa wizi na ghasia wakati wa safari yao, inasema WFP, ambayo pia inahofia magonjwa ya mlipuko wakati wa msimu wa mvua.
Baada ya kupata uhuru kutoka kwa Sudan mwaka 2011, Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya takriban watu 400,000 na mamilioni kuyahama makazi yao kati ya 2013 na 2018.