Wataalamu wa utunzaji wa mazingira wamesema idadi ya wanyama, ndege na samaki duniani imepungua kwa zaidi ya theluthi mbili mnamo kipindi cha miaka 50 iliyopita, kutokana na matumizi ya binadamu yaliyokithiri.
Katika ripoti ya wataalamu hao iliyochapishwa leo Alhamisi, wamesema binadamu wameharibu robo tatu ya eneo la nchi kavu na asilimia 40 ya bahari, na wameonya kuwa kiwango hiki cha uharibifu wa mazingira kitakuwa na athari zisizoelezeka kwa afya za binadamu na maisha kwa ujumla.
Ripoti hiyo ijulikanayo kama Faharasa ya Sayari Hai ya mwaka 2020, imesema ufyekaji wa misitu na kilimo ni shughuli mbili zilizoongoza kuangamiza asilimia 60 ya viumbe hai kati ya mwaka 1970 na 2016.
Nusu karne iliyopita, imetahadharisha ripoti hiyo, imeshuhudia maendeleo makubwa kiuchumi, ambayo yameambatana na mahitaji makubwa ya rasilimali asilia.