Mashahidi 109 wanatarajia kutoa ushahidi wao katika kesi inayomkabili mfanyabiashara, Mohamed Yusufali na wenzake Wawili baada ya kusomewa maelezo ya mashaidi na vielelezo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Yusufali na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtaka 39 ikiwemo kuisababishia serikali hasara ya Sh.Bil 2 lakini wakati wakisomewa maelezo ya mashahidi yaliongezwa na kufikia mashtaka 45.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Alloyscious Gonzaga Mandago na Isaac Wilfred Kasanga.
Wakili wa Serikali Mkuu,Neema Mwanza, Pendo Makondo,Tumaini Kweka na Leonard Swai kutoka Takukuru waliwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo washitakiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Miongoni mwa mashahidi hao ni Msajili Msaidizi Mwandamizi wa Brela,Seka Isaya Kasera, Afisa kodi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Dickson Chiguo na Kaimu Afisa Biashara Manispaa ya Kinondoni, Abdul Abeid Issa.Mbali na mashahidi hao, pia vielelezo 75 zikiwemo nyaraka na barua mbalimbali vitatolewa mahakamani hapo.
Hatua hiyo ya kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo washtakiwa hao, imehitimisha na kufungwa katika Mahakama ya Kisutu ambapo jalada la kesi hiyo sasa lehamishiwa rasmi Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, na litapangiwa tarehe kwa ajili ya kuanza kutoa ushahidi.