Kituo cha watoto yatima katika mji mkuu wa Sudan kimehamishwa kufuatia vifo vya zaidi ya watoto 70 wachanga, na watoto wakubwa kutokana na njaa na magonjwa katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto na shirika la misaada la ndani lilisema Jumatano.
Mkasa huo katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Al-Mayqoma uligonga vichwa vya habari mwishoni mwa mwezi uliopita wakati mapigano yakiendelea kati ya wanajeshi wa Sudan na Wanajeshi wa Msaada wa Haraka.
Vifo hivyo vimeangazia idadi kubwa ya raia tangu katikati ya mwezi wa Aprili wakati mapigano yalipozuka kati ya vikosi vinavyomtii Jenerali Abdel-Fattah Burhan na vikosi vya RSF vinavyoongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo.
Takriban watoto 300 katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Al-Mayqoma mjini Khartoum walihamishiwa “mahali salama” mahali pengine katika taifa hilo la kaskazini-mashariki mwa Afrika, alisema Ricardo Pires, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.
Wizara ya maendeleo ya jamii na afya ya Sudan imechukua jukumu la kuwasimamia watoto hao, huku UNICEF ikitoa msaada wa kibinadamu ikiwa ni pamoja na matibabu, chakula, shughuli za elimu na michezo, Pires alisema katika barua pepe kwa The Associated Press.
Alisema watoto hao wamefanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kufuatia safari yao ndefu kuelekea eneo lao jipya, na kuongeza kuwa “mtoto yeyote anayehitaji kulazwa hospitalini atapata huduma ya afya.”