Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu linasema lina wasiwasi na ukame unaozidi kuwa mbaya nchini Ethiopia na linahitaji fedha zaidi ili kuongeza juhudi za kukabiliana na hali hiyo.
Ukame umeathiri watu milioni nne katika mikoa yenye migogoro ya Amhara na Oromia, pamoja na Afar na Tigray, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilisema Jumatano.
“Migogoro mingi na mara nyingi inayoingiliana imedhoofisha sana uwezo wa watu wa kukabiliana na majanga ya hali ya hewa kama vile ukame – na kuacha mamilioni ya watu wakiwa katika hatari ya kutumbukia katika uhitaji mkubwa na ufukara,” Shirika hilo limesema
Serikali kuu mjini Addis Ababa hapo awali iliondoa hofu ya kutokea baa la njaa, na imesema kuwa inajitahidi kutoa misaada.
Wiki hii, mamlaka ya Tigray ilifichua kuwa zaidi ya watu 200 walikufa kwa njaa, baada ya onyo mwezi uliopita kwamba eneo hilo “liko karibu na janga la kibinadamu”.