Wananchi mkoani Njombe wametakiwa kulipa kodi ya pango la ardhi ndani ya siku 30 kama ilivyoelezwa na Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa kuwa “wananchi wote wanaomiliki viwanja na ambao hawajalipa pango la kodi ya ardhi, wanapaswa walipe kodi hiyo kuanzia tarehe 10/05/2024.”
Wito huo umetolewa na Kamishina wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Njombe Fulgence Kanuti ambapo amesema kulipa kodi kwa hiari kutaondoa usumbufu na wananchi ambao watashindwa kulipa kwa muda uliotolewa watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kushitakiwa na kubatilisha milki za viwanja vyao.
Aidha emesema kuwa “Katika kipindi cha siku 30 Ofisi ya Kamishina wa Ardhi mkoa na Ofisi za Ardhi za Halmashauri zote ndani ya mkoa wa Njombe zitakuwa wazi mpaka saa 2:00 usiku na wananchi wafike katika ofisi hizo kwa ajili ya kupata ankara za madai (control number) ili kurahisisha ulipaji wa kodi ya pango la ardhi”
Ameongeza kuwa zoezi hilo ni la muda wa siku thelathini hivyo wananchi ambao bado hawajalipa wafike katika Ofisi za Ardhi za Halmashauri za mkoa wa Njombe na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi kulipa kodi hiyo.