Leo October 31 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameondoka nchini kuelekea Nairobi nchini Kenya kwa ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini humo kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Rais Magufuli ameagwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es salaam, Paul Makonda na viongozi mbalimbali wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Mara baada ya kuwasili nchini Kenya, Rais Magufuli atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, na baadae atakwenda kutoa heshima katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta.
Rais pia anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa atakayoandaliwa na mwenyeji wake Ikulu Jijini Nairobi. Katika ziara hiyo Rais Magufuli anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha Eldoville kilichopo Karen Jijini Nairobi na pia kuzindua barabara mchepuko (Southern By-pass) iliyopo Jijini humo. Barabara hiyo ni moja kati ya miradi mikubwa ya barabara nchini Kenya, inayounganisha maeneo mbalimbali ya Jiji la Nairobi kwa barabara za juu na chini.
ULIKOSA HII YA RAIS MAGUFULI ALIVYOFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA WIZARA YA MALIASILI? UNAWEZA KUANGALIA VIDEO HII HAPA CHINI