Wasuluhishi wa migogoro ya kibiashara nchini na wahitimu wa mafunzo ya utatuzi wa migogoro ya kibiashara, wameonywa kuhusu rushwa na kutakiwa kuwa chachu ya usuluhishi wenye mafanikio, kwa faida ya biashara zao na uchumi wa taifa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wakitoa mafunzo kuhusu mbinu bora za kutatua migogoro ya kibiashara kwa washiriki wa mafunzo hayo DSM mwishoni mwa wiki, waelimishaji wabobezi wa masuala ya usuluhishi, chini ya Mpango wa Mafunzo wa Baraza la Ujenzi la Taifa (NCC) wamesema, rushwa ni kikwazo.
Mhandisi Samwel Msita na Wakili Rosan Mbwambo wamewataka washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia maadili, miongozo, sheria, kanuni na miiko ya usuluhishi, huku wakilenga kuimaliza kwa amani ili biashara zisikwame.
Mhandisi Msita aliyekuwa wa kwanza kutoa elimu hiyo amesema, “Ukiwa msuluhishi mpenda fedha utajikuta ukiuendeleza mgogoro badala ya kuumaliza, kwa sababu hutasimamia haki. Nawasihi wapenda hela kuwa makini na rushwa”.
Amesema ni vyema wakati wowote wanapohitajika kutatua migogoro ya kibiashara, hata kama ni kwenye biashara zao, wasimamie haki na kuangalia namna bora ya kuzifanya pande zilizoingia kwenye mgogoro kuelewana na kuendeleza biashara.
Amesema katika biashara kuna kodi ya nchi inayopaswa kulipwa, hivyo wasuluhishi lazima wawe makini kuhakikisha kupenda kwao fedha hakuwapeleki kuithamini rushwa na kuitengenezea mazingira ya ushindi zaidi ya kutatua migogoro iliyombele yao.
“Ikiwa ni kwenye eneo la manunuzi, msuluhishi zingatia sheria za manunuzi na wala usilete zakwako au kuzipindisha zilizopo kwa faida yako. Tunachokitaka ni kuona unafikiwa muafaka wenye mafanikio,”Msita
Kwa upande wake, Wakili Mbwambo alisema, siku zote msuluhishi wa mgogoro wa kibiashara anapaswa kuepuka rushwa na sababu nyingine zinazoweza kumfanya abadili kanuni, sheria na miiko ya usuluhishi, kuepuka kuupendelea upande mmoja.
Kwa mujibu wa Mbwambo, migogoro ya kibiashara inaposhindwa kumalizwa inazuia wahusika kuendelea kufanya biashara, hivyo wasuluhishi wanapaswa kuhakikisha wanawapatanisha huku kila upande ukipata haki yake unaoidai na wala si kuendeleza mivutano inayopoteza muda.
Kutokana na maelezo yake, lengo la usuluhishi wa kibiashara ni kuwaacha walio kwenye mgogoro wa kibiashara wakiwa marafiki wenye uwezo wa kuendeleza biashara kwa amani na kuchangia kukuza uchumi wa nchi.
WANZANIA MIL 29 KUPIGA KURA OCTOBA 28, IDADI YA WENYE ULEMAVU YAONGEZEKA