Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa usimamizi mzuri wa Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kilichopo jijini Dodoma.
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Mhe. Japhet Hasunga baada ya kutembelea na kukagua mradi huo pamoja na wajumbe wa kamati hiyo leo tarehe 23 Januari 2025.
Hasunga ameitaka TANROADS kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa miundombinu ya kiwanja hicho ili kuweza kukamilika kwa wakati na ubora uliokusudiwa.
“Tumefurahi na tumeona maendeleo mazuri ya ujenzi wa kiwanja hiki kikubwa, tunampongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huu mkubwa ambao ameufanya.
“Ili tuweze kupima thamani ya fedha lazima tujue ni lini uwanja huu utakamilika na ukamilike kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa na kuanza kutumika, tunatamani kufikia mwezi wa saba uwe umekamilika,” alisisitiza Hasunga.
Aidha Hasunga ameongeza kuwa, “Eneo la kiwanja hiki ni kubwa lenye zaidi ya hekali elfu 11 hivyo litengwe eneo litakalotumika kwa ajili ya ujenzi wa hoteli, kumbi za mikutano na maduka makubwa (shopping malls) ili kuendelea kukuza utalii na kuchangamsha Uchumi wa Mkoa wa Dodoma”.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma Mhe. Jackline Ngonyani amepongeza jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita Pamoja na TANROADS kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa kiwanja hicho.