Kinda hatari wa klabu ya Chelsea, Cole Palmer anaamini kwamba uamuzi wake wa kuondoka katika klabu ya utotoni ya Manchester City na kujiunga na Chelsea umezaa matunda baada ya kutajwa kwenye kikosi cha Uingereza kwa mara ya kwanza.
Palmer, 21, alijiunga na The Blues kwa dili la kushtukiza la pauni milioni 42.5 msimu wa joto na kuanza maisha mazuri London kwa bao la kusawazisha dakika ya 96 dhidi ya klabu yake ya zamani siku ya Jumapili, na kufuatiwa na kuitwa kwenye kikosi cha Gareth Southgate cha England.
Mshambulizi huyo analenga kucheza mechi yake ya kwanza ya wakubwa katika mchezo wa Ijumaa dhidi ya Malta katika uwanja wa Wembley au ziara ya Kaskazini mwa Macedonia siku ya Jumatatu, wakati England inakamilisha kufuzu kwa Ubingwa wa Uropa msimu ujao.
Palmer alifichua kuwa aliwaza mfululizo kwa “siku chache” baada ya Chelsea kukaribia lakini anasema aliamua kuhama kwa ajili ya kazi yake.
“Ilikuwa hatua kubwa kwangu, sijawahi kutoka Manchester, hata kwa mkopo au kitu kama hicho, kwa hivyo kuhamia huko peke yangu lilikuwa jambo kubwa,” alisema.