Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani ameonya kuhusu uwezekano wa kutokea vita vya nyuklia duniani.
Papa Francis alitoa indhari hiyo jana Jumanne katika mkutano a kimataifa wa Oslo na kueleza kuwa: Dunia ipo katika ncha ya kutumbukia kwenye vita vya nyuklia, kama ilivyoshuhudiwa kwenye mgogoro wa makombora ya Cuba mwaka 1962.
Amesema, “mkutano huu unafanyika, huku dunia yetu ikiendelea kukabiliwa na hatari ya kutokea Vita vya Tatu vya Dunia, na huku mgogoro wa Ukraine ukitokota, bila ya uwepo wa mikakati ya kuondoa hatari ya silaha za nyuklia.”
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani amesema dunia ambayo ipo salama na huru kutokana na silaha za nyuklia ni jambo la dharura na linalowezekana.
Mwezi uliopita pia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alionya kuhusu uwezekano wa kutokea vita vya nyuklia duniani. Antonio Guterres alisema katika ujumbe wake kwamba, wakati huu ambapo baadhi ya nchi zinatishia kutumia silaha za nyuklia, kivuli cha vita vya nyuklia kinaonekana tena kwenye sayari ya dunia.