Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameiombea Haiti inayokabiliwa na machafuko yanayoendeshwa na magenge ya wahalifu yenye silaha.
Papa Francis ameombea kumalizika kwa machafuko hayo na kutoa wito kwa pande zote kushirikiana ili kupata amani na maridhiano, wakati kukiwa na mwitikio mpya wa msaada wa jamii ya kimataifa.
“Ninafuatilia kwa wasiwasi na maumivu makubwa mzozo unaoliathiri taifa la Haiti pamoja na mawimbi ya machafuko yanayotokea hivi karibuni huko” , amesema Papa Francis.
Maelfu ya wafungwa wamekuwa huru baada ya magenge kuvamia jela na kuwaachia huru, katika nchi yenye serikali isiyo na afisa hata mmoja aliyechaguliwa na raia na kiongozi wa genge ambaye anamtishia waziri mkuu waziwazi.
Matukio yanayoendelea nchini Haiti yanawashtua hata wale wanaofuatilia kuongezeka kwa makundi yenye silaha nchini humo katika miaka ya hivi karibuni.