Papa Francis aliruhusiwa kutoka hospitali ya Roma ya Gemelli Ijumaa ambapo mzee huyo mwenye umri wa miaka 86 alikuwa akipata nafuu kutokana na upasuaji wa tumbo, baada ya upasuaji huo kuzua wasiwasi juu ya afya yake.
Papa aliondoka hospitalini akiwa katika kiti cha magurudumu na kuzungumza na watu na wafanyakazi wa afya waliokuwa wamekusanyika nje ya lango la kuaga.
Watu pia walipanga mstari nje ya kituo hicho kwa nia ya kumuona papa, ambaye alitabasamu na kuwapungia mkono wale waliokuwa wakisubiri.
Alizingirwa na ulinzi huku akiondoka na kusaidiwa kuingia kwenye gari lililokuwa likimsubiri. Francis alipigwa picha akisali katika Basilica ya Santa Maria Maggiore katika mji mkuu wa Italia mara baada ya kuachiliwa kwake.
Papa mwenye umri wa miaka 86 amekumbwa na msururu wa changamoto za kiafya tangu kuchaguliwa kwake mwaka 2013 kuhudumu katika nafasi hiyo, kutokana na matatizo ya nyonga, maumivu ya goti na maambukizi ya mfumo wa kupumua.
Papa alifanyiwa upasuaji wa saa tatu Juni 7 ambapo hii ilikuwa ni mara yake ya tatu kukaa hospitalini tangu 2021.