Kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis, hapo jana alitangaza kuteua makadinali wapya 21, wakiwemo maaskofu kutoka Jerusalem na Hong Kong, ambako kuna wakatoliki wachache, akiacha alama nyingine kwa kanisa kwa kuteua makadinali ambao watachagua mrithi wake ikiwa atafariki au kujiuzulu.
Sherehe ya kutangazwa kwa makadinali hao itafanyika Septemba 30, ambapo kundi hilo litakuwa la tisa kuundwa chini ya papa Francis ambaye amekuwa akiongoza kanisa katoliki kwa muda wa miaka 10.
Uteuzi wa makadinali hawa unatazamwa kama ishara ya mustakabali wa baadaye wa kanisa katoliki dunaini lenye waumini takriban bilioni 1.3.
Makadinali 18 kati yao na ambao wako chini ya miaka 80 wanatarajiwa kushiriki katika zoezi la kumteua mrithi wa papa Francis baada ya kifo au kustaafu kwake.
Makadinali hao wapya wanatoka katika nchi mbalimbali zikiwemo Mareknai, Italia, Argentina, Afrika Kusini, Uhispania, Sudan Kusini, Tanzania, Colombia, Poland na Ureno.