NIPASHE
Mbunge wa zamani wa Jimbo la Korogwe Vijijini, Mussa Lupatu ni miongoni mwa waliofariki katika ajali ya mabasi mawili na gari ndogo iliyotokea kijiji cha Mkata Tanga.
Kaimu Kamanda wa Polisi Tanga, Juma Ndaki amesema Marehemu Lupatu alipata ajali hiyo akitokea Kibaha kuelekea Korogwe kumpeleka mwanae kupatiwa matibabu ya ugonjwa akili ambaye naye pia alifariki.
Wengine waliyotajwa kufariki katika ajali hiyo ni karani wa Mahakama ya Ardhi Dar es Salaam, Devota Msimbe ambaye alifariki wakati akikimbizwa Hospitali ya Muhimbili.
Kamanda Ndaki alisema maiti tatu bado hazijatambuliwa na miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya Magunga Korogwe, majeruhi 12 bado wamelazwa katika Hospitali tofauti.
Majeruhi 12 kati ya 34 wamelazwa katika hospitali tofauti, wakiwamo saba waliopelekwa Muhimbili, mmoja hospitali ya wilaya ya Handeni na wanne kituo cha afya Mkata, wilayani Handeni.
NIPASHE
Watu wanaoishi Vigwaza, wilaya ya Bagamoyo wameamua kuwaajiri watoto wao waliomaliza kidato cha nne kufundisha Shule ya Msingi Visezi, ili kutatua tatizo la upungufu wa walimu shuleni hapo huku wakiwalipa posho ya sh. 15,000 kwa wiki.
Wananchi hao wamesema wanawalipa watoto hao Sh. 15, 000 kwa wiki kama posho ya kujikimu.
Walisema wameamua kuajiri watoto wao baada ya kuona wamekuwa na changamoto hiyo kwa aidi ya miaka 10 na hakuna juhudi zozote zinazofanywa na serikali kutatua tatizo hilo.
“Ngoja tukwambie, sisi wanavisezi wote ni wanaCCM kwa hiyo usiwe na wasiwasi lakini kama hutatatua hizi kero zetu CCM itashinda kwa shida sana, sio siri,”—alisema Mwenyekiti wa kijiji hicho, Hamisi Kiatala.
“Kero ya walimu itakwisha hivi karibuni.. TAMISEMI wana mpango wa kuwaajiri walimu, lakini viongozi wa kijiji hamjawahi kuniambia hizi kero zenu wakati mimi ni mbunge wenu pia ndio waziri mwenye dhamana… hizi kero zinazowezekana kutatua nitazitatua kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji, zitakazoshindikana tutazishughulikia mwakani kama nitarudi tena”, alisema Kiatala.
HABARI LEO
Kusambaa kwa taarifa kuwa kuna uwezekano wa kutokea kwa shambulio la kigaidi katika miji ikiwemo Dar na Mwanza kumefanya baadhi ya Taasisi kama vyuo vikuu na TANESCo kuchukua tahadhari kwa kuweka taarifa ya tahadhari na kuelekeza namna hatua za kufanya ili kujiepusha na kujilinda.
“Kutokana na tishio hilo, tumeona ni vyema tuchukue hatua mapema.. si lazima yatokee ndivyo tuchukue hatua, tumeona ni vyema kujihami kwa kuimarisha ulinzi katika vituo vyetu..”—Mkurugenzi wa TANESCo, Felchesmi Mramba.
Baadhi ya tahadhari walizozichukua Taasisi hizo ni wafanyakazi na wanafunzi kuvaa vitambulisho vyao wakati wote, ukaguzi wa wageni na watu wote wanoingia maeneo ya Taasisi hizo, pamoja na kuwekwa kwa matangazo ya tahadhari katika maeneo hayo.
Jeshi la Polisi limeonywa watu kuacha tabia ya kutunga na kusamba ujumbe kwenye simu na mitandao ya kijamii unaowatia hofu wananchi.
MWANANCHI
MWANANCHI
Wajawazito Wilaya ya Kishapu Shinyanga wamelalamikia kujifungua kwa kutumia tochi za simu na huku wengine wakilazimika kwenda na lita ya mafuta ya taa ili wapate mwanga wa taa pamoja na pia moto wa kuchemshia vifaa kutokana na kukosa umeme katika Zahanati.
“Kituo chetu tunapokea kwa wajawazito 12 kwa siku kwa siku ambao hufika kujifungua kila siku na wagonjwa wanaofika kujifungua kwa sasa. Pia tatizo jingine hapa ni vyoo.. hivi vilivyopo vinaanguka wakati wowote.. hata daktari wa Kituo hana Choo”—alisema Muuguzi msaidizi wa Zahanati hiyo, Ruth Mabula.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mohammed Mlewa amesema wamepata ufadhili wa kutoka Japan ambao watafunga umeme wa jua katika Zahanati hiyo.
MWANANCHI
Hali ya taharuki, hekaheka na tafrani ilitanda Kituo cha Mabasi cha Ubungo na sehemu nyingine jijini Dar na mikoani wakati madereva wa mabasi walipofanya mgomo wa saa tisa kuishinikiza Serikali kufuta matumizi ya kanuni mpya za udhibiti wa safari na usalama huku barabara mbalimbali zikifungwa.
Askari walijikuta wakilazimika kutumia mabomu ya machozi huku viongozi wa Jeshi la Polisi wakipuuzwa wakati wakijaribu kutuliza madereva wa magari ya mikoani kuachana na mgomo huo kwa maelezo kuwa madai yao yanashughulikiwa.
Hali ilikuwa mbaya zaidi kwenye vituo vya daladala ambako hakukuwa na mabasi na kulazimisha wananchi wengi kutembea kuelekea makazini.
Hali ilitulia na kubadilika kuwa shangwe saa 7:30 mchana baada ya Waziri wa Kazi, Ajira na maendeleo ya Vijana, Gaudensia Kabaka kutangaza kufutwa kwa matumizi ya kanuni hizo mpya, huku kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akitangaza kusitishwa kwa tochi maalum za kung’amua mwendo wa mabasi na kuondolewa kwa vituo vya ukaguzi.
Mgomo huo ulitokana na Serikali kuifanyia marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani kwa kuingiza kipengele kinachowataka madereva kwenda Chuo cha Usafirishaji (NIT) kwa mafunzo ya muda mfupi mara kila wakati leseni zao zinapoisha ili kupata sifa ya kupata leseni nyingine utaratibu ambao ulitangazwa mwezi Machi 2015.
Madai mengine waliyogomea madereva hao pia ni kuhudhuria mafunzo hayo wakati hawana mikataba ya ajira inayoweza kuwahakikishia kazi zao zinalindwa hadi wanapomaliza mafunzo pamoja na kudai kuondolewa kwa faini ya Sh300,000 kwa kila kosa la barabarani.
Baada ya hali kuzidi kuwa mbaya waziri Kabaka alilazimika kwenda Ubungo 6:15 mchana akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
Maeneo mengine yaliyotajwa kuguswa na mgomo huo ni pamoja na Mbeya, Mwanza, Kahama, Kagera, Geita, Shinyanga na Tabora.
NIPASHE
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme TANESCo, Felchesmi Mramba amewahakikishia Watanzania kuwa hakuna mgawo wa umeme huku baadhi ya maeneo wakilalamika kukatiwa bila taarifa yoyote kutoka TANESCo.
Mkurugenzi huyo amesema taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari ni kuwepo kwa matengenezo ya kisima cha Songas ambayo hufanyika kila mwaka na tayari matengenezo yameanza huku Shirika lilihakikisha hakuna athari yoyote kwa wananchi.
Mramba amesema TANESCo ina vyanzo vingi vya umeme vya kujitosheleza kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa wateja wake.
Mramba alisema hali ya umeme kwa hivi karibuni imeathiriwa na mvua zilizonyesha kwa mfululizo na kusababisha madhara katika nguzo za umeme.
“Hakuna mgawo wa chini chini wala wa juu juu tulihakikisha katika matengenezo ya kisima hicho cha Songas hapatatokea athari yoyote,” alisema Mramba.
millardayo.com ndio sehemu yako kuzipata story zote mtu wangu, unaweza kuwa karibu zaidi na mimi kwa kujiunga kwenye Facebook, Twitter na Instagram pia zitakufikia zote mtu wangu, jiunge hapa >>>twitter Insta Facebook