MWANANCHI
Aliyekuwa Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu aliyeamua kulitema taji hilo baada ya kubebeshwa kashfa amesema kuna wakati alitaka kujiua lakini alirudisha moyo nyuma na kuona ingekuwa shida kubwa nyumbani kwao.
“Sikuwa na amani, niliishi maisha ya hofu, kujifungia ndani, kulia wakati wote. Ilifikia hatua baba yangu alipata mshktuko kiasi cha kwenda kutibiwa Afrika Kusini. Mama yangu pia alipata mshtuko…ningeweza kumpoteza.”—Sitti Mtemvu.
“Mama yangu alisali na mimi, alinipigania, hakuonyesha hadharani jinsi gani anaumia, lakini ukweli ni kwamba nilimwona alivyokuwa anadhoofu na kukosa raha. Nyumba yetu iligeuka sehemu ya huzuni, amani ilitoweka ni kama tulikuwa na msiba.”—Sitti Mtemvu.
Sitti anasema siku moja mama yake alimwambia kwamba aliumia siku alipompoteza mama yake lakini machungu aliyoyasikia kwa Sitti ni mazito zaidi japo baba yake wakati wote alivumilia na hakuonesha maumivu yake.
Anasema kuna wakati baba yake alikwenda Afrika Kusini na akiwa huko alimtumia ujumbe wa kumuomba msamaha na alimwambia kwamba hizo ni changamoto.
Sitti anasema alikuwa katika wakati mgumu kiasi cha kufikia uamuzi wa kutupa laini yake ya simu ya zamani.
MWANANCHI
Jina la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere limeibuka ghafla na kwa nguvu baada ya makada wa CCM kuanza kutangaza nia, huku wengi wao wakionesha kuaminiwa na muasisi huyo wa Taifa na wengine kuahidi kufuata miiko aliyoiweka wakati alipoongoza Serikali ya Awamu ya Kwanza.
Makada wengine wametembelea kaburi la Baba wa Taifa na wengine kutumia kuaminiwa kwake na wananchi wakati akiwa na umri mdogo ili kujenga hoja kuwa uzoefu na umri si suala la kuzingatiwa katika kupata kiongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Mwalimu Nyerere alikuwa na nguvu ya ushawishi na mkali dhidi ya rushwa na ufisadi jambo lililomfanya aheshimike ndani na nje ya nchi.
Miezi michache baada ya Bunge la Katiba kuondoa mambo ya maadili kwenye Rasimu ya Katiba, suala hilo linaonekana kurudi kwa nguvu kwenye sera za wagombea uongozi ambao wanataja kila mara jina la Nyerere, miaka 16 baada ya kifo chake.
“Wanamtumia Nyerere kwa sababu wanajua alikuwa muadilifu, alikuwa akisema kitu watu wanatekeleza. Leo kiongozi anatoa maagizo hakuna anayetekeleza,” alisema mchungaji wa Kanisa la Pentekoste, Dk Damas Mukasa.
Mmoja wa Makada hao, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema kuwa anatosha kushika wadhifa huo na kwamba Mwalimu Nyerere atafurahi huko aliko iwapo atachaguliwa kuwa Rais kwa miaka 10 ijayo.
Membe alisema kuwa Machi mwaka huu alikwenda Butiama na kuzuru kaburi la Mwalimu Nyerere ambako alipiga magoti na kumweleza nia yake ya kuutaka urais.
Mkurugenzi mkuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk Hassy Kitine naye alitumia jina hilo wakati akitangaza nia ya kutaka kurejea Ikulu ambako alifanya kazi chini ya utawala wa muasisi huyo, akiahidi kutumia miaka mitano kuirudisha Tanzania ya Mwalimu Nyerere.
Dk Kitine alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake aliyoitoa mjini Dodoma kutoa mifano ya utendaji wa Mwalimu Nyerere na kuwaponda wengine waliojitokeza kuwa hawana sifa za kumfikia.
HABARI LEO
Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha INTEPOL wamefanikiwa kuwakamata watu 141 kwa makosa mbalimbali katika Oparesheni iliyofanyika kwa siku mbili.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, CP Diwani Athumani amesema baadhi ya makosa ambayo watu hao wamekamatwa yapo makosa ya wizi wa magari, dawa za kulevya, silaha haramuna milipuko, wahamiaji haramu na biashara haramu ya binadamu pamoja na wizi wa miundombinu ya umeme na nyara za Serikali.
Katika magari 1,400 yaliyokaguliwa, magari sita yaligundulika kuwa ya wizi na mengine matano yalichezewa chesisi pamoja na pikipiki 12 nazo ziliibiwa.
Kati ya magari yaliyoibiwa, matatu yalitoka England, moja kutoka Hungary na jingine kutoka Tanzania.
HABARI LEO
Diwani wa Kata ya Kigamboni amesema wana mpango wa kujenga uzio kuzunguka Shule mbalimbali zilizopo kwenye Kata hiyo ili kukabiliana na tatizo la utoro wa Wanafunzi.
“Eneo la Shule linatakiwa liwe salama ndio maana tunazijengea uzio, pia kutapunguza tatizo la utoro kwa wanafunzi na kuongeza ufanisi wa Shule hizo”—Dotto Msawa, Diwani wa Kigamboni.
Diwani huyo amesema ujenzi huo utaanza muda sio mrefu kwa kuwa tayari Mkandarasi amepatikana na kinachosubiriwa ni kuypitishwa kwa Bajeti ya Serikali 2015/16.
NIPASHE
Waziri Stephen Wassira ambaye pia ametangaza nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema yeye ndiye anayefaa kuwa rais wa nchi kwa sababu anaichukia rushwa na hana kashfa yoyote.
Alisema nchi hii kwa sasa imejaa wala rushwa na kwamba yeye ataikomesha kwa sababu anaichukia wala hajawahi kuiomba au kuipokea, huku akisema kuwa kuna wanachama wenzake, ambao ni wala rushwa wakubwa na kila kashfa wanaguswa lakini sasa wanataka waingie Ikulu kwa kutumia rushwa waliyoivuna wakiwa madarakani.
Aidha, alisema akibahatika kuingia tano bora na kisha tatu bora na badaye akapeperusha bendera ya CCM kama mgombea wa urais kupitia tiketi ya chama hicho, ni lazima viongozi wa Ukawa watajinyonga kwa sababu wanamtambua jinsi alivyo na uwezo.
“Ukienda hospitali utakutana na rushwa, polisi rushwa na mahakamani rushwa… Rushwa imeanza zamani maana hata yule aliyekuwa akibeba mikoba ya Yesu, lakini alivyopewa vipande 30 vya fedha akamsaliti Yesu, kwa hiyo rushwa ni tatizo haikuanza leo, bali ya leo imezidi sana, ipo nyingine ya mikataba mibovu, manunuzi, sasa akiwa Rais ambaye ni mla rushwa atawaonea aibu wenzake.”—Waziri Wassira.
Alisema atahakikisha jembe la mkono kwa wakulima linakuwa historia, ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira kwa vijana, kingine ni kuboresha elimu ya sayansi kwa wanafunzi wa sekondari.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.