MWANANCHI
Wakati Mkutano wa Bunge ukianza kwa mjadala wa uliopoteza mwelekeo na kutawaliwa na malumbano kati ya Wabunge wa CCM na wa Vyama vya Upinzani, Naibu Spika Job Ndugai amesema ni vigumu hali hiyo kuzuilika kwa kuwa mwaka huu ni mwaka wa Uchaguzi.
Bunge hilo lilipokea na kuanza kujadili Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo yaliibuka malumbano ya kisiasa huku Wabunge wa Upinzani wakilalamikia udhaifu wa Serikali katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa miaka 10 iliyopita.
“Mwaka huu ni wa Uchaguzi huwezi kuzuia hiyo hali na kumbuka kuwa Wabunge ni Wanasiasa.. Wabunge homa zipo juu na hawawezi kukaa hapa wakati katika Majimbo yao wanapigiwa simu kuwa yamevamiwa”—Naibu Spika Job Ndugai.
Baadhi ya Wabunge walisema agenda kuu kwa sasa ni Uchaguzi Mkuu kwa kuwa hiki ni kikao cha mwisho cha Bunge na baada ya hapo wote wanarudi Majimboni kwa ajili ya Uchaguzi.
MWANANCHI
Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe imewabana walimu wa Shule ya Sekondari ya Msimbu na kuwataka waandike barua kujieleza baada ya kushika nafasi ya mwisho Kiwilaya katika matokeo ya Kidato cha Pili na kidato cha nne 2014.
Mkurugenzi wa Wilaya hiyo, Mwamvua Mrindoko alisema waliunda Kamati kuchunguza sababu ya kufeli huko.
Mrindoko amesema baadhi ya sababu walizobaini kuchangia kufeli kwa wanafunzi wengi iko ya ushirikiano duni kati ya shule na Jamii, msukumo mdogo wa wazazi kwenye elimu pamoja na utoro wa wanafunzi.
MWANANCHI
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amewasili Bujumbura ikiwa ni siku mbili baada ya waasi kutangaza kumuondoa madarakani na tayari majenerali watatu waliotangaza mapinduzi wamekamatwa huku wanajeshi 12 wakiuawa.
Kulikuwa na taarifa kuwa kiongozi wa uasi huo, Meja Jenerali Godefroid Niyombare alikuwa amekamatwa pamoja na wasaidizi wake, lakini baadaye mshauri wa habari wa rais, Willy Nyamwite alisema alipewa taarifa zisizo sahihi.
Hata hivyo waasi hao wamesema wataendeleza vita dhidi ya majeshi ya Serikali kwa ajili ya kumuondoa Rais huyo ambaye anapingwa kutokana na kutangaza kugombea urais kwa mara ya tatu kinyume na katiba.
Msafara wa Rais Nkurunziza ulioneshwa kwenye televisheni ukiwasili Bujumbura, ingawa picha hizo hazikumuonyesha Rais huyo ambaye alipitia kijijini kwake Ngozi kabla ya kwenda jijini humo akitokea Tanzania.
Wanajeshi 12 wa upinzani waliuawa wakati wa mapambano ya kuwania kituo hicho juzi.
Wanajeshi wengine 35 wa uasi walijeruhiwa na 40 wamejisalimisha huku wanajeshi wanne wa Nkurunziza wakijeruhiwa.
Hali ya jijini Bujumbura ilikuwa shwari jana baada ya mapambano kutawala siku nzima ya juzi wakati majeshi yanayomtii Nkurunziza yalipokuwa yakipambana kukomboa sehemu muhimu.
Baada ya kuwasili Rais Nkurunziza alipewa taarifa fupi ya mapinduzi na hata jinsi jeshi lilivyofanikiwa kuzima uasi.
NIPASHE
Kutokana na machafuko yanayoendelea Burundi na kusababisha kufurika kwa waomba hifadhi mkoa wa Kigoma, kambi ya Nyarugusu imejaa na kusababisha shule zilizopo ndani ya kambi hiyo kufungwa kwa muda.
“Kwa kawaida kambi hii ina uwezo wa watu 50,000 kulingana na taratibu za kimataifa, lakini mpaka sasa ina wakimbizi 54,706…hivyo baada ya kuanza kuwapokea waomba hifadhi wapya Aprili 29, mwaka huu, tumepata wapya 16,808 hadi juzi”– alisema Mkuu wa kambi hiyo, Sospeter Boyo.
Alisema kwa sasa wamefunga shule ili majengo hayo yatumike kuwahifadhi wahamiaji wapya wanaowasili kila siku huku wakifanya jitihada kupata sehemu nyingine ya kuwahifadhi.
Baadhi ya wakimbizi kambini hapo, walisema kitendo cha kushindwa kuondolewa madarakani kwa Rais Pierre Nkurunzinza, kimewasikitisha kwani kitasababisha kuwapo na machafuko zaidi.
“Tunasikitika sana kwa jaribio hilo kutofanikiwa, sasa hali itakuwa mbaya zaidi nchini kwetu kutokana na machafuko ya kushindwa kuondolewa madarakani Nkurunzinza”– alisema mmoja wa wakimbizi hao.
Wakimbizi hao wamesema Demokrasia ndani ya Burundi imepotea na pia kunafanyika mauaji ya kimya kimya kwa wananchi wenye mlengo tofauti na Rais aliyepo madarakani.
NIPASHE
Mbunge Suleiman Said Bungara ‘Bwege’ ametofautiana na wabunge wenzake wa upinzani wanaosema Serikali ya CCM imechoka, badala yake amesema Watanzania ndio waliochoka huku akisema kuwa wapo wabunge wanaoitetea serikali kwa kuibeba, lakini wapo wabunge wanaofanya kazi zao za kuikosoa.
Bwege alisema serikali haijachoka kama wengine wanavyosema isipokuwa waliochoka ni Watanzania wanaoibeba serikali hiyo wamechoka, wamejiandaa kuiondoa madarakani katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu na kuwaweka wagombea wa UKAWA madarakani.
“Fungeni virago muondoke… anakuja Mbunge hapa na kusema serikali imejenga shule, Zahanati halafu baadaye wanaomba/wanalalamika miradi ya maendeleo katika majimbo yao haijatekelezwa.. Wabunge wa CCM wamechoka, wanajiaga wenyewe”—Suleiman Bwege.
Hoja ya kuchoka kwa Serikali ya CCM ilitolewa na Mbunge Tundu Lissu akiituhumu serikali hiyo kwa kushindwa kuwaletea wananchi maendeleo.
Tangu siku hiyo wabunge wengi wa upinzani wanaochangia hotuba ya Waziri Mkuu wamekuwa wakitumia lugha hiyo huku Wabunge wa CCM wakijitutumua kuitetea kuwa haijachoka.
MTANZANIA
Mbunge Gosbert Blandes ametishia kumfanyia kitu kibaya Mkuu wa Wilaya Karagwe, Dari Rwegasira akidai anawapendelea wahamiaji haramu toka Rwanda huku akiwanyanyasa wananchi.
“DC huyu ni bomu, ni mzigo… yeye anafanya kazi huku mwili ukiwa Tanzania lakini roho yake ikiwa Rwanda, ninaomba Serikali msiwe mnatuletea watu waliochoka kiasi kile.. kama hamtamwondoa mtaona tutakachokifanya”—Mbunge Gozibert Blandes.
Mbunge wa Viti Maalum, Rose Kigirini alisimama kuomba mwongozo kutokana na kauli iliyotolewa na Mbunge huyo na baadae Waziri Jenista Mhagama alisimama na kusema kuwa Serikali imesikia kuhusu ombi la Mbunge huyo na watalifanyia kazi.
TANZANIA DAIMA
Mbunge Edward Lowassa ametuma salamu za kwa wagombea wenzake wa Urais kupitia CCM baada ya kuwek wazi kuwa atatangaza rasmi kugombea nafas hiyo Mei 24 mwaka huu huku akiwaomba wakazi wa Arusha kujitokeza kwa wingii katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid ili kumuunga mkono kwenye safari yake ya matumaini.
“Nimefurahi nimekuja wiki moja kabla ya jambo hilo.. nataka nije niseme neno, nitasema neno ambalo nitaomba mniunge mkono.. nninataka kila mwana Arusha ajitokeze, mtu akikuuliza unakwenda wapi mwambie ninakwenda kwenye safari ya matumaini”—Edward Lowassa.
Mbunge Lowassa amesema hayo katika harambee iliyofanyika Arusha ambapo alimwakilisha Makamu wa Rais, Gharib Bilal.
Katika harambee hiyo jumla ya pesa zilizochangishwa ni Mil. 254 ambazo zitatumika kwenye ujenzi wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa uliopo Tengeru.
JAMBO LEO
Wingu la uhaba wa nyama limetanda Dar baada ya machinjio ya Ukonga na Vingunguti kufungwa kutokana na kukithiri kwa uchafu huku machinjio nyingine za Mbagala na Tegeta nazo zikifungwa kwa sababu hiyohiyo.
Hatua ya kufungwa kwa machinjio imeonekana kuwa pigo kwa wafanyabiashara ambao ni zaidi ya 3,000 huku wengi wao wakiwa vijana.
Hatua ya kufungwa kwa machinjio hizo kumewashangaza wafanyabiashara hao ambao wamedai wanatoa ushuru ambao ni zaidi ya mamilioni kila siku lakini maeneo ya machinjio hizo bado kumekithiri uchafu.
“Ni vigumu kusema tunafunga kwa muda gani ila tutafanya haraka iwezekanavyo kufuatilia suala hilo kuhakikisha kuwa usafi unafanyika”—alisema Taibu Shaibu, Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.