Mbunge Godbless Lema amesema Kambi ya upinzani italazimika kujilinda katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu endapo polisi wataendelea kutumiwa kisiasa na kuwaacha green guards wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya fujo kwenye mikutano yao.
Lema amesema UKAWA wametoa tahadhari kwa CCM endapo wamepanga njama zozote kuhujumu vyama vyao katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
“Njama hizo zitadhibitiwa ipasavyo kwa sababu upinzani wa sasa hivi una nguvu kuliko wakati mwingine wowote”—Godbless Lema.
Mbunge huyo amesema taifa linaelekea kwenye uchanguzi mkuu, kipindi ambacho amani ya nchi inatakiwa kulindwa kwa nguvu zaidi kuliko vipindi vingine.
Alisema kwa kipindi chote cha miaka 10 ya serikali ya awamu ya nne, kambi ya upinzani imepigia kelele na kulaani mauaji ya raia wasio na hatia yanayofanywa na vyombo vya dola ikiwemo polisi.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi Zanzibar linawashikilia watu wawili kwa kesi ya kuwakashifu na kutishia kuangamiza familia za viongozi wakuu wa Serikali ikiwemo Rais Dk. Shein, Makamu wake wa Pili, Balozi Seif Idd na watendaji wengine.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Salum Msangi amesema watu hao walitumia simu za mkononi kusambaza ujumbe wa sauti na picha kwenye mitandao ya Facebook na Whatsapp ukiwa na ujumbe wa shutuma juu ya viongozi hao.
Mmoja ya watuhumiwa hao alituma ujumbe wa vitisho kwamba Rais Dk. Shein na Balozi Seif Idd wasiende Pemba kwa kuwa hakuna wafuasi wa CCM na kama chama hicho kikishinda basi watazichoma moto nyumba za Askari Polisi waliopo kisiwani humo.
Polisi wanaendelea kuwahoji watu hao na kama wakikutwa na hatia watapandishwa Mahakamani.
MTANZANIA
Mbunge Rebecca Ngodo amelalamikia maji ya wilaya ya Meru kuwa yana madini ya Fluoride ambayo yanachangia kuwaharibu meno wakazi wa maeneo hayo.
Mbunge huyo alihoji Bungeni kuwa Serikali ina mpango gani kuwasaidia wakazi wa eneo hilo kuhusu maji hayo ambayo yanasababisha meno kubadilika rangi kuwa ya kahawia na miguu kuwa na matege.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla alisema tatizo hilo liko katika Mikoa mingi ikiwemo Singida, Mwanza na Arusha na pia Serikali inafanya utafiti ili kupata njia ya upunfuza madini ya Fluoride katika maji hayo.
NIPASHE
Tatizo la unywaji pombe wa kupindukia kwa wanaume Wilaya ya Rombo limechukua sura mpya baada ya jeshi la polisi Kilimanjaro kutuhumiwa kushiriki kuchochea biashara hiyo ambapo Mkuu wa Mkoa huo, Leonidas Gama alisema kuwa taarifa mbali mbali zinaonyesha kuwa baadhi ya askari si waaminifu katika vita dhidi ya pombe haramu.
“OCD taarifa zinaonesha kuna baadhi ya askari wako, ambao wanashirikiana na wafanyabiashara wa pombe haramu ya gongo na hili linafanya kazi ya operesheni kukomesha tabia hii mbaya kuwa ngumu,”—RC Leonidas Gama.
Alisema kuna taarifa kuwa wapo baadhi ya askari wasio waaminifu wamewageuza wafanyabiashara wa gongo kuwa ATM zao kwa kuchukua rushwa hivyo kusababisha uovu huo uendelee.
“Inasikitisha kusikia kuwa baadhi ya pombe zinazonyweka Rombo zimetengenezwa na mbolea aina ya urea, maji ya betri, spiriti, kinyesi cha binadamu, sukari guru na molasesi, hii ni hatari kwa afya ya mwanadamu,”—Leonidas Gama.
Suala la ulevi uliokithiri limekuwa gumzo maeneo mbali mbali mkoani Kilimanjaro na nje ya mkoa huo ambapo imedaiwa kuwa baadhi ya wanawake wilayani humo wanalazimika kukodi wanaume kutoka nchi jirani ya Kenya ili kukidhi mahitaji yao ya kindoa.
Elizabeth Shabani na Mary Shirima ni baadhi ya wakazi wa Wilaya hiyo ambapo wamekiri kuwapo kwa askari, wanaofika maeneo wanapotengenezea pombe haramu kuchukua fedha kila mwisho wa mwezi kama ni ujira wa kuwalinda.
HABARI LEO
Waziri Dk. Hussein Mwinyi amesema vijana wote waliomaliza kidato cha sita 2013/14, 2014/15 na kutojiunga na mafunzo ya JKT wanaendelea kusakwa na wanaorodheswa kwenye watoro wa Jeshi na upo uwezekano wakapelekwa kwenye mafunzo mwezi ujao.
Waziri huyo amesema utaratibu wa kuwapeleka wahitimu hao uko kisheria kabisa na unalenga kuwajengea uzalendo, ukakamavu, maadili mema, utaifa na kutoa stadi za kazi.
Waziri Mwinyi amesema vijana waliomaliza kidato cha sita ni 41,000 lakini walioenda ni wachache na waliotoroka wanaorodheshwa kama watoro wa Jeshi na Serikali inaangalia namna ya kuwapeleka kwa mkupuo kuanzia mwezi Agosti.
MWANANCHI
Safari ya Zitto Kabwe kurejea Bungeni imeanza rasmi baada ya kiongozi huyo wa chama cha ACT-Wazalendo kuchukua fomu za kuwania kuongoza jimbo la Kigoma Mjini.
Uamuzi huo wa kulitaka jimbo hilo unathibitisha kauli zake ambazo amekuwa akizitoa kwa muda mrefu kuwa hatarudi tena Kigoma Kaskazini kwa kuwa alishawatimizia kila kitu na haoni sababu za kuwawakilisha tena wananchi wa eneo hilo.
Kauli yake iliibua ubashiri kuwa Zitto anataka kubadilishana jimbo na mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, uvumi ambao aliukanusha akisema hadhani kama CCM inaweza kupata jimbo Kigoma.
Zitto hakufanya mbwembwe wakati akienda kuchukua fomu kwenye ofisi za ACT Ujiji jana, badala yake aliita viongozi wa kata na matawi bila ya kutaarifu vyombo vya habari.
“Nimeamua kugombea ubunge wa Kigoma Mjini ili niwatumikie ndugu zangu ambao wamekuwa wakipata tabu katika kupigania haki zao za msingi ambazo walistahili kuzipata kama ilivyo katika mikoa mingine,” alisema Zitto alipoongea na mwandishi wa gazeti la Mwananchi kwa simu.
“Nakusudia kuibana Serikali ijenge skimu ya umwagiliaji maji ili wakulima walime kilimo cha mpunga kwa mwaka mzima bila kupumzika, jambo ambalo litainua uchumi wa wakulima na kuongeza chakula hapa Kigoma,”—Zitto Kabwe.
Katibu wa ACT wa Jimbo la Kigoma Mjini, Azizi Ally alisema Zitto alichukua fomu hiyo jana kwa malipo ya Sh 100,000 mbele ya viongozi 72 wa kata na matawi kutoka jimboni humo.
MWANANCHI
Mpambano mkali wa kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea Urais kupitia CCM sasa umeanza rasmi baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kuwaweka huru makada sita waliokuwa wamefungiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja kwa makosa ya kukiuka kanuni za uchaguzi.
Kufunguliwa kwa makada hao, ambao baadhi yao wanapewa nafasi kubwa ya kupitishwa na chama hicho kumekuja wakati CCM ikikabiliwa na tishio la kutokea mgawanyiko mkubwa, hasa kutokana na baadhi ya kambi kuituhumu sekretarieti kuwa inabagua baadhi ya wagombea.
Makada waliofungiwa tangu February 2014 kwa kosa la kuanza kampeni mapema ni mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, pamoja na Mawaziri Bernard Membe, Steven Wasira, January Makamba na mbunge William Ngeleja.
Baadhi ya wanachama wa CCM, hasa wajumbe wa Halmashauri Kuu, walianza kumiminika nyumbani kwa makada hao baada ya kupata taarifa za kuondolewa kwa adhabu hiyo, wengi wakionekana kwenda kumpongeza Lowassa.
“Nimefurahishwa na uamuzi wa Kamati Kuu. Safari ya ushindi sasa inaanza,”—January Makamba.
“Hatua inayofuata ni kuhakikisha kwamba nafuata kanuni, taratibu na miongozo ya chama katika kugombea nafasi nitakayoiomba,”—William Ngeleja.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.