NIPASHE
Muuguzi mmoja wa zahanati ya Muungano, Dodoma amekumbwa na kashfa nzito baada ya kudaiwa kumchapa viboko mama mjamzito ambaye alikuwa na hali ya uchungu wa kujifungua na kusababisha mtoto aliyetaka kujifungua kufariki akiwa tumboni.
Mwanamke huyo, Mariamu Maroda amedaiwa kulazwa kwenye ICU kwa zaidi ya wiki moja, ambapo pamoja na kufanyiwa upasuaji, hakufanikiwa kupata mtoto wake akiwa hai.
“Nilishuhudia Lucy akimchapa Maroda viboko kwenye mapaja na mgongoni, akisema ana uwezo wa kujifungua lakini anadeka tu, nilishindwa kuingilia nikihofia asimdhuru zaidi mwanangu, ila nilihuzunika sana,” alisimulia mama mdogo wa Maroda, Joyce Charles.
Alisema muuguzi huyo alitumia fimbo tatu kumchapa mgonjwa wake, fimbo zilipomalizika, alianza kumfinya mwanamke huyo kwenye mapaja kwa kutumia rula.
“Kesho yake saa 12:00 alfajiri, huku hali ya mgonjwa ikiwa mbaya, walitupatia gari likatupeleka hospitali ya Mvumi Misheni, ambako walisema hali aliyokuwa nayo mgonjwa wasingeiweza na kutuelekeza tumpeleke hospitali ya rufaa, lakini walimpa mgonjwa chupa mbili za damu.. ukimuona, mwilini ana alama za fimbo na kufinywa”— Joyce Charles.
Viongozi wa Hospitali ya Rufaa, wenye mamlaka ya kuzungumzia suala hilo walionekana ‘kurushiana mpira’ walipotakiwa kuelezea suala hilo.
Hata hivyo, Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anatoria Mkindo alikiri kuwepo kwa mgonjwa huyo lakini Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Zainab Chaula alisema hakuwa na taarifa kuhusu Maroda.
Mdogo wa Maroda, Silika Mkwawi amesema ingawa hakuingia kwenye chumba cha kujifunguli, dada yake alipotolewa nje, muuguzi alimwambia kuwa alimchapa fimbo mbili tu, kwa sababu ya kudeka kwake.
HABARI LEO
WATU 20 wamekamatwa na Polisi baada ya kumjeruhi askari aliyekuwa doria na mwenzake.
Kamanda wa Polisi Morogoro, RPC Leonard Paul amesema watu 20 watu hao walimshambulia kwa kumpiga na kitu butu kichwani askari wa jeshi hilo, Koplo Ramadhani ambapo baada ya kupigwa alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro ambako amelazwa na anaendelea vizuri na matibabu.
Kamanda huyo amesema pikipiki isiyofahamika namba za usajili iliyokuwa ikiendeshwa na Juma Abasi, mkazi wa Mindu iligonga gari aina ya Isuzu Tipper kusababisha majeraha kwa mpanda pikipiki huyo, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa mwendesha pikipiki kuingia barabarani bila kuchukua tahadhari.
Hata hivyo alisema ajali hiyo ilishuhudiwa na askari hao waliokuwa doria na pikipiki maeneo hayo, walifika eneo la ajali ili kutoa msaada na katika harakati hizo za kutoa masaada ndipo askari Koplo Ramadhani alipopigwa na kitu butu kichwani na watu waliotokea eneo hilo na kuanguka chini.
MTANZANIA
Utafiti umeonesha kuwa wanaume wenye umri kati ya miaka 40-50 wapo katika hatari kubwa ya kujiua kutokana na msongo wa mawazo unaowatokea kwa sababu tofauti huku wengi wakikosa washauri.
Utafiti huo ulifanywa Uingereza baada mzee mmoja kujiua siku yake ya kuzaliwa akiwa na umri wa miaka 44.
Utafiti unaonesha ndani ya wiki moja wanaume 100 hujiua huku idadi hiyo ikiizidi ya wanawake wanaojiua kwa zaidi ya mara nne.
Professa mmoja Kiongozi wa Kituo cha Utafiti Chuo cha Glasgow amesema tabia ya kujiua ni tatizo la kisaikolojia linalotokana na upungufu wa kiakili.
MWANANCHI
Mwili wa mwanafunzi wa kidato cha pili aliyefariki kwa Manyara umezikwa jana huku Mchungaji wa Anglikana akiwataka ndugu wakubaliane na hali iliyotokea.
“Tunaiomba Serikali namna ya walimu wanavhottoa adhabu.. kifo hicho kimesababishwa na uzembe”—Mchungaji Noel Bichima.
Ndugu na jamaa waliokuwa kwenye mazishi hayo walionesha kusikitisha sana na kitendo cha mwanafunzi huyo kuchapwa hadi kufariki wakisema kuwa ni ukatili.
Walimu watatu wamekamatwa wanashikiliwa na Polisi wakidaiwa kusababisha kifo cha mwanafunzi huyo.
MTANZANIA
Hali ya ulinzi katikati ya DAR imeonekana sio ya kawaida baada ya Askari wa Jesh la Polisi kuonekana kutanda huku wakiwa na silaha mbalimbali.
Baadhi ya maeneo ambayo imeonekana ulinzi huo kuimarika ni pamoja na Mlimani City, Posta na Namanga huku magari ya Polisi yakiendelea kuzunguka maeneo mbalimbali ya Jiji.
Gazeti la MTANZANIA liliwasiliana na Kamanda Kova ambaye amesema hali hiyo imetokana na operesheni maalum ya kupambana na uhalifu.
“Hii inaitwa High Police Visibility tunajua kwamba uwepo wa mwonekano wa Askari kwa wingi unasaidia kupunguza uwezekano wa kutokea uhalifu”—Kamanda Kova.