HABARILEO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki ameitaka Idara ya Uchambuzi na Ushauri wa Kazi – Utumishi, kuwianisha mishahara ya watumishi wa wakala za Serikali, ili kusiwe na tofauti kubwa kati ya watumishi wa juu na wa chini.
Kairuki alisema hayo jana alipoitembelea idara hiyo, ikiwa ni muendelezo wa ratiba yake ya kutembelea idara/ vitengo vya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
“Katika baadhi ya wakala za Serikali kuna tofauti kubwa ya mshahara kati ya watumishi wa juu na wa chini, hivyo ningependa tuangalie namna ya kuwezesha watumishi wa chini, ili wawe na morali ya kufanya kazi,” alisema Waziri Kairuki.
Aliitaka idara hiyo kuhakikisha wakala zote za Serikali, zinawasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu yao zinazostahili kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Utumishi, ili Serikali ijue namna zinavyojiendesha.
“Hakikisheni taarifa zinazohitajika Ofisi ya Rais-Utumishi zinawasilishwa kwa wakati, ili tubaini upungufu uliopo na kufanyia kazi kwa lengo la kuboresha huduma kwa umma,” alisisitiza Waziri Kairuki.
HABARILEO
Dereva wa basi la Allys Star, Alfa Haji (37) lililokuwa likitokea katika wilaya ya Kaliua kuelekea jijini Mwanza amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Urambo mkoani Tabora, akikabiliwa na mashitaka 22 ikiwemo kusababisha vifo vya watu wanane na majeruhi 13.
Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Hassani Momba, Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi Mkaguzi Msaidizi, Felibet Pima alisema kwamba Desemba 15 mwaka huu, saa 12:00 asubuhi katika kijiji cha Vumilia wilaya ya Urambo mtuhumiwa huyo aliendesha gari kizembe na kusababisha vifo vya watu wanane.
Alisema kwamba licha ya kusababisha vifo vya watu wanane pia akiendesha gari kwa uzembe alisababisha majeruhi kwa watu 13. Mwendesha mashitaka huyo aliwataja marehemu waliotambuliwa kuwa ni Hamisi Ramadhani mkazi wa Magili mkoani Tabora, Grace Andrew (24), ambaye ni mkazi wa Ng’ambo Tabora, Paschal Abdul (miezi 8) mkazi wa Bunda,Tipwege Kataga (20), Emeliana Tryphon (24) , Antoni Julius Mkazi wa Wilayani Kaliua, Shija Anton mkazi wa Kaliua na Rahel Mussa Mkazi wa Ulyankulu wilayani Kaliua.
Aidha Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi, Pima aliwataja majeruhi mbele ya Mahakama hiyo kuwa ni Pili Juma (15), Maro Machano (50), Gift Mayunga (29), Ibrahimu Hasani (25), Rahel Mabula (20) Jane Inosent( 29) Anges Michael na Godlifa Alois (35). Wengine ni Santo Lufasiza (28) Mariamu Cosmas (38) Fatuma Juma (19) Yunge Sini (9) na Marthar Luhende (21).
Hata hivyo mtuhumiwa huyo alikana mashitaka yote 22 na amerudishwa rumande baada ya Mahakama kuona ni njia ya kumpatia usalama wake na kesi hiyo itatajwa tena Desemba 31 mwaka huu.
NIPASHE
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imesema kuwa mwaka huu Tanzania, imekuwa na kiwango cha juu zaidi cha joto ikilinganishwa na miaka mingine hususan katika jiji la Dar es Salaam na Zanzibar.
Aidha hali hiyo ya hewa inatajwa kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa kote duniani, ikiwamo kiwango cha mvua za elnino katika Bahari ya Pacific.
Kiwango cha juu cha joto jijini Dar es Salaam ni kati ya nyuzi joto 33-35 huku Zanzibar ikiwa ni kati ya 27-32.
Meneja wa Huduma za Utabiri wa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA), Samwel Mbuya aliiambia Nipashe jana jijini Dar es Salaam.
Alisema mvua hizo za elnino zimesababisha unyevunyevu kuongezeka katika mkondo wa Bahari ya Hindi hivyo Pwani ya bahari hiyo kuwa na joto kali.
Mbuya alisema tayari Shirika la Hali ya Hewa Duniani(WMO), limetangaza kuwa mwaka huu ni mwaka joto kali zaidi duniani kote.
Alisema kiwango cha joto kwa mikoa ya Pwani kimeongezeka zaidi kuanzia Desemba Mosi mwaka huu.
“Pamoja na mikoa ya ukanda wa Pwani kuwa na mvua bado joto ni kali tofauti na mikoa mingine isiyo ukanda huu mvua zikinyesha hali ya hewa inakuwa ni nyepesi,”alisema Mbuya
NIPASHE
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesisitiza kuwa atasimamia kushuka kwa bei ya umeme kwa namna yoyote ile.
Alitoa ahadi hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza masuala mbalimbali yanayohusu nishati ya umeme na namna wazawa wanavyoweza kuwekeza kuzalisha umeme.
Alisema idara na taasisi zilizo chini yake zinapaswa kukutana kutafuta majibu ya kudumu ya matatizo ya upatikanaji wa umeme wa uhakikia kwa sasa na kwa miaka 10 hadi 20 ijayo.
Alisema wafanyabiashara pamoja na wawekezaji wa ndani wanakaribishwa kuwekeza katika sekta ya nishati.
Profesa Muhongo alisema Tanzani ina vyanzo vingi vya upatikanaji wa umeme, hivyo kwa yoyote ambaye anahitaji ni ruksa kuwekeza katika sekta hiyo ili kuongeza nishati hiyo.
“Kama nilivyowahi kusema huu umeme wa Megawati 1,400 hautoshi inabidi kuuongeza mara kumi ili ifikapo 2025 tuwe nchi yenye kipato cha kati kwa kuwa na umeme wa zaidi ya Megawati 10,000, kampuni ambazo zinaweza kuzalisha umeme wa Megawati 100, 200, 500, 1000… mnakaribishwa kuwekeza,” alisema.
Waziri huyo alisema wawekezaji hao wanatakiwa kuwekeza katika vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme ikiwemo, gesi, makaa ya mawe, miradi mikubwa na midogo ya maji, nishati ya jua, upepo, jotoardhi, umeme wa mabaki ya taka, Bayogesi na Umeme wa mawimbi.
NIPASHE
Kasi ya kutumbua majibu ya Rais, John Magufuli imeanza kuwageukia wakurugenzi wa halmashauri na manispaa nchini ikiwa ni utekelezaji wa alivyoahidi kwenye Uchaguzi Mkuu uliomwingiza madarakani kwamba hatahamisha mtendaji mbovu.
Hatua ya serikali ya Dk. Magufuli kumwondoa kazini aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Musa Natty ni salamu tosha kwa wakurugenzi wengine kwamba mambo aliyoaahidi kwenye kampeni zake hazikuwa mbwembwe za kuwafurahisha wapiga kura wake.
Baada ya kashfa ya mkataba wa uendelezaji wa ufukwe wa Coco Beach, harakaharaka Tamisemi ilimhamishia Natty Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mjini, mkoani Manyara, lakini juzi Ikulu ilimwamuru Mhandisi huyo kurejea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusubiri uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.
Hatua hiyo ya Ikulu kumwondoa kazini Natty ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Magufuli kwenye kampeni zake kwamba watumishi wenye kashfa na wasiotimiza wajibu wao ipasavyo hawatahamishwa bali watafukuzwa kazi.
Kwenye kampeni zake, Dk. Magufuli mara kwa mara alikuwa akisisitiza kuwa hatafanya mchezo wa kuwahamisha hamisha watendaji wabovu kama ilivyozoeleka kwenye awamu zilizopita na badala yake mtumishi atakayeharibu sehemu moja atakuwa ameharibu maisha yake yote.
Katika serikali za awamu zilizopita ilikuwa kawaida kwa wakurugenzi na maofisa wengine hasa wa halmashauri na manispaa kuhamishiwa mikoa na wilaya zingine wanapoharibu kazi ama kukumbwa na kashfa mbalimbali.
Dk. Magufuli alikuwa akisisitiza kuwa Tanzania inawasomi na wazalendo wengi wa kuitumikia nchi yao hivyo hatakuwa na sababu ya kumhamisha mtumishi mbovu kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine.
Ahadi hiyo ya Dk. Magufuli inaonekana kuanza kumgusa moja kwa moja Mhandisi Natty, ambaye sasa amepoteza kazi na anasubiri uchunguzi wa tuhuma dhidi yake ili afikishwe mahakamani itakapobainika kuwa alihusika.
Tuhuma anazokabiliwa nazo Natty ambazo zimekuwa maisha ya kawaida kwenye halmashauri na manispaa nyingi nchini ni pamoja na ujenzi wa barabara usio kuwa na viwango, migogoro ya ardhi, uuzaji wa maeneo ya wazi hali inayosababisha migogoro kwenye maeneo mbalimbali.
Mfano, Dk. Magufuli alipozungumza na wakazi wa Nyamongo na Tarime, kwenye kampeni zake lisema serikali yake itakomesha tabia ya kuhamisha hamisha watendaji wabovu wa serikali walioharibu sehemu moja kwenda nyingine na badala yake watafukuzwa kazi moja kwa moja.
Alisema tabia hiyo imekuwa ikichanagia kwa kiwango kikubwa kuchelewesha maendeleo ya wananchi na kuahidi kuwa utaratibu huo utafika mwisho iwapo atachaguliwa kuingia Ikulu.
“Unakuta mtu kaharibu Tarime anapelekwa Mwanza, akiharibu Mwanza anahamishiwa Tanga, kwenye serikali yangu hakutakuwa na utaratibu mbovu kama huo, ukiharibu sehemu moja ujue umeharibu maisha yako yote, kwangu ni kazi tu ukiondoka umeondoka hakuna kuhamishwa,” alisema
Pia Dk. John Magaufuli, aliahidi kukomesha tabia ya wakurugenzi wa halmashauri manispaa kulipana posho zisizo na maana wakati miradi ya maendeleo ikiendelea kukwama.
Akiwa katika jimbo la Bukene mkoani Tabora katika ziara zake za kujinadi alisema watumishi wa halmashauri mbalimbali wamekuwa wakilipana posho mbalimbali kwa ajili ya safari zisizo na msingi wakati fedha hizo zingesaidia miradi ya maendeleo.
“Kwenye halmashauri nyingi safari za kila aina haziishi wanajipa posho wakidai kwenda wiki ya maji wakati maji yenyewe hakuna, wengine wanajipa posho kwenda wiki ya maziwa wakati wananchi hawanyi maziwa, mara utasikia wiki ya nyama ilimradi kutafuna fedha za wananchi,” alisema Dk. Magufuli.
NIPASHE
Mkuu wa Idara ya Ulinzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Emil Kisamo, ameuawa kinyama na watu wasiojulikana kwa kukatwa shingo na kisha kufungiwa ndani ya buti ya gari lake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Libaratus Sabas, alisema jana kuwa tukio hilo linadhaniwa kutokea kati ya alfajiri ya kuamkia Ijumaa saa 3:00 asubuhi.
Alisema tukio hilo lilitokea eneo la Lemara jijini hapa.
Kamanda Sabas alisema awali kabla ya kubaini kuwepo kwa tukio hilo, wananchi wa eneo hilo walitoa taarifa za kuwepo kwa gari namba T 435 CSY likiwa limefungwa milango yote na kutelekezwa katika eneo lao kuanzia asubuhi hadi jioni.
Kwa mujibu wa Kamanda Sabas, baada ya kupata taarifa hizo walifika eneo la tukio na kujiridhisha kuwa gari hilo lilikuwa limetelekezwa na wauaji hao.
Alisema walilivuta hadi kituo cha polisi na kuanza kumtafuta mwenyewe wakati huo wakiwa hawajui kuwa kuna mtu kwenye buti.
Kamanda Sabas, alisema wakati wanaendelea na zoezi la uchunguzi wa sababu za kutelekezwa kwa gari hilo na kumpata mwenyewe siku ya pili yaani jana, mke wa marehemu alijitokeza na kuitambua gari hiyo kuwa ilikuwa ni ya mumewe.
Aliendelea kufafanua kuwa mumewe huyo alitoka asubuhi ya Desemba 18 mwaka huu, kwa madai ya kwenda kufuatilia taratibu za safari yake ya kwenda nje ya nchi kwa matibabu.
Alisema tangu wakati huo hakurudi licha ya kuwa simu ya kiganjani ilikuwa inaita bila kupokelewa.
Kamanda Sabas alisema walimuomba alete funguo za akiba za gari ili walifanyie ukaguzi na walipofungua kwenye buti ndipo wakamkuta Kisamo akiwa amekufa na akiwa na jeraha la kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni upande wa nyuma.
Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na imewaomba wananchi kutoa ushirikiano.
MWANANCHI
Jiji la Dar es Salaam lilisimama kwa muda wakati wa ukaguzi wa mradi wa mabasi yaendayo kasi, uliofanywa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiandamana na viongozi mbalimbali wa Serikali na baadhi ya wadau wa usafirishaji nchini huku akitoa maagizo saba.
Katika ziara hiyo iliyochukua takriban saa tatu, Waziri Majaliwa alipita katika vituo vyote vilivyopo kwenye mradi huo, akitaka kujua ni wapi utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa, Novemba 27, mwaka huu ulipoishia.
“Tena ingekuwa vizuri kama vituo hivi vyote vingefungwa viyoyozi ili kuboresha mandhari pindi wanaposubiri usafiri,” alisema Wazri Mkuu Majaliwa kwenye ziara hiyo.
Akitoa maagizo yake alimwita mhandisi, Frank Mbilinyi kutoka Tanroads akimtaka ahakikishe vigae vilivyokuwepo kwenye kituo hicho vinabadilishwa kabla ya kuzinduliwa kwa mradi huo Januari 10 mwakani.
“Nilipokuja mara ya kwanza nakumbuka tulikubaliana kuwa vigae hivi havina ubora, hivyo naagiza viondolewe mara moja,” alisema. Aliwataka kujenga uzio kwenye kituo cha Kivukoni kwa lengo la kulinda usalama wa abiria lakini pia miundombinu.
“Hakikisheni kunakuwa na uzio, nafikiri nyote mnakijua kituo cha mabasi cha Msamvu Morogoro, kina geti moja la kuingilia na moja la kutoka. Hivyo nafikiri ni vizuri kuiga mfano wao,” alifafanua. “Enhe kuna vyoo?” aliuliza wakati akiendelea na ukaguzi huu kabla ya kujibiwa na Asteria Mlambo ofisa mtendaji mkuu wa Darts.
Karakana ilikuwa ina idadi ya mabasi yapatayo 140, yakijumuisha mabasi madogo na makubwa.
Kwa mujibu wa Asteria Mlambo, mabasi makubwa yatakuwa yakitumia njia maalumu zilizojengwa na Darts, ambapo hata utaratibu wake wa ukatishaji tiketi ni tofauti na ule wa yale ya kawaida.
“Mabasi ya kawaida yatakuwa yakichukua abiria kutoka maeneo ya ndani na kuwaleta kwenye vituo vya mabasi yaendayo kasi” “utaratibu wa ukatishaji tiketi kwenye mbasi madogo ni kama huu wa kawaida uliozoeleka,” alisema.
Lakini kwa upande wa yale makubwa, utaratibu wa ukatishaji tiketi utakuwa ni ndani ya gari ambapo abiria atajihudumia mwenyewe.
Pia atakuwa na uwezo wa kukata tiketi ya kutumia hata mwaka mzima kulingana na mahitaji yake. Baada ya kutoka kwenye karakana msafara huo moja kwa moja ulifika Kimara, ambapo alipoingia tu, alipokewa na wakazi wa eneo hilo wakipaza sauti kuhusiana na tatizo la maji linalowakabili.
Hata hivyo Waziri Majaliwa alitoa ahadi kuwa angelitafutia ufumbuzi tatizo hilo, kabla ya kuto agizo la nne kwa watendaji wa Darts kuhakikisha kuwa vituo vyote vya mradi huo vinakamilisha ujenzi wa uzio , lakini pia kunakuwa na milango maalumu yenye uwezo wa kujifunga na kujifungua, ili kurahisisha huduma kwa abiria watakaokuwa wakitumia usafiri huo.
Waziri Mkuu Majaliwa katika agizo lake la tano aliwataka wadau wanaohusika na mfumo wa ukatishaji wa tiketi wahakikishe Serikali inanufaika na mradi huo.
Agizo la sita lilikwenda moja kwa moja wa wanasheria wa Tamisemi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha mikataba yote imekamilika. “Fanyeni mapitio ya mikataba yote na uendeshaji wake na namna ya mfumo wa utendaji wake utakavyofanya kazi na kwa kuwa mtakutana kama Waziri Simbachawene (George), ni vyema mkahakikisha Serikali inalindwa,” alisisitiza.
Pia Waziri Majaliwa alitoa agizo lake la saba katika ziara yake akiitaka manispaa ya Kinondoni kuhakikisha inajenga eneo la maegesho, wakitafuta eneo hilo kwa gharama yoyote ile ili kuondoa tatizo la msongamano wa magari linalolikabili jiji la Dar es Salaam.
Alisema kuliko kuruhusu magari ishirini yaliyobeba watu ishirini, ni vyema watu hao wakaegesha magari yao kwenye maegesho yatakayojengwa katika eneo maalumu
MWANANCHI
Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa amesema anashangaa kuona anaambiwa mleta vurugu wakati dunia inamkubali kuwa ni mlinzi wa amani.
Kauli ya Lowassa imekuja ikiwa ni siku moja baada ya taasisi za kidini 1,200 duniani kupitisha jina lake kwa ajili ya kumpatia Tuzo ya Amani.
“Nimepokea kwa unyenyekevu na furaha tuzo ya amani duniani ninayotarajiwa kupewa na taasisi za kidini 1200 duniani,” alisema Lowassa akinukuliwa na msemaji wake, Aboubakar Liongo.
Lowassa alisema tuzo hiyo ni kithibitisho cha uongo wa CCM na Serikali yake kuwa wapinzani ni watu wa vurugu. Taasisi hizo katika kikao chake huko Bukavu DR Congo, zilitangaza kumpa tuzo hiyo Edward Lowassa kutokana na utulivu aliyouonyesha kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu Kwa jamii, Mchungaji William Mwamalanga ilisema kiasi wajumbe 1,400 wa mkutano huo kutoka kote duniani walikubaliana kumpa tuzo hiyo Lowassa kati ya wanasiasa 1,000 waliyoshindanishwa ili kumpata kiongozi bora wa Amani mwaka 2015, ambaye anajali na kuangalia maslahi ya jamii badala ya madaraka.
Alisema yeye ni muungwana na ana hofu ya Mungu na hata siku moja hatoweka mbele maslahi binafsi, na ndiyo maana aliwatuliza wananchi waliyokuwa wakimtaka kutoa tamko baada ya matokeo kutangazwa.
“Siko tayari kuingia Ikulu huku mikono yangu ikibubujika damu. Nashukuru taasisi hizo za kidini duniani, zimeliona hilo,” alisisitiza Lowassa
MWANANCHI
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema Rais amempa kazi ya kuhakikisha anakamilisha mchakato wa Katiba Mpya pamoja na uanzishwaji wa Mahakama ya Rushwa.
Kura ya Maoni ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa ilipangwa kufanyika Aprili 30, lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikatangaza kuiahirisha hadi itakapotangazwa tema, ikisema inataka kukamilisha kwanza uandikishaji wapigakura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25.
Lakini kabla ya kutangaza kuahirisha kazi hiyo, vyama vya upinzani, ambavyo vilisusia Bunge la Katiba kwa madai kuwa lilikiuka utashi wa wananchi kwa kuweka kando sehemu kubwa ya mapendekezo yaliyokuwa kwenye Rasimu ya Katiba, walikuwa wakitaka mchakato huo uanze upya.
Lakini jana, Dk Mwakyembe alisema moja ya majukumu aliyopewa ni kuhakikisha anakamilisha mchakato huo wa kuunda Katiba Mpya ulioanza miaka mitatu iliyopita wakati Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alipotangaza kuanza rasmi kuwa Serikali itaanza kazi ya kuandika Katiba Mpya.
“Kuna masuala mengi ambayo wizara yangu inahusika nayo, mengine bado sijayaelewa vyema kwamba yapo kwenye hatua gani, lakini suala la Katiba Mpya hilo ni jukumu ambalo hata Rais alinitamkia kuwa amenikabidhi niliendeleze kwa hatua iliyobaki,” alisema Dk Mwakyembe alipozungumza na Mwananchi.
Kauli yake Dk Mwakyembe ambaye amebobea kwenye sheria, haikupokelewa vizuri na wanasiasa wa upinzani ambao walisema kutekelezwa kwa mpango huo kutakuwa ni kuanzisha tena mgogoro bila ya sababu za maana, na kwamba upatikanaji wa kura za Wazanzibari walioko Bara bado haujapatiwa ufumbuzi.
Akizungumzia tamko hilo la Dk Mwakyembe, mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema ikiwa Serikali inataka kuendeleza mchakato wa Katiba, ikubali kuunda upya Bunge la Katiba kwa mujibu wa sheria.
“Sheria ya Kura ya Maoni haina utaratibu wa kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya na hairuhusu kupata tarehe mpya ya kupiga kura ya maoni baada ya kuahirisha upigaji kura,” alisema mwanasheria huyo wa kujitegemea.
“Kama Mwakyembe ataendeleza upya mchakato huu, aanzie alipoishia Jaji (Joseph) Warioba.” Bunge la Katiba liliingia dosari baada ya wajumbe kutoka vyama vinne vya Chadema, NLD, CUF na NCCRMageuzi na wengine kutoka taasisi tofauti, kususia vikao wakidai kuwa mapendekezo ya wananchi yaliyokuwa kwenye Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Katiba, ambayo iliongozwa na Jaji Joseph Warioba, yalitupwa na badala yake yakawekwa mapendekezo ya CCM.
Wajumbe hao walitoka wakati Bunge la Katiba likiwa limekwama kwenye Sura ya Kwanza na ya Sita zinazozungumzia Muundo wa Muungano, baada ya Tume ya Warioba kuwasilisha mapendekezo yanayotaka serikali tatu, huku wajumbe wengi wa chombo waliotoka CCM wakitaka uendelee muundo wa sasa wa serikali mbili.
Pamoja na wajumbe wa vyama hivyo vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kujiengua, Bunge la Katiba liliendelea na mchakato na kufikia kupitisha Katiba inayopendekezwa ambayo ingepigiwa kura na wananchi Aprili 30, lakini haikuwezekana.
“Kwanza Bunge la Katiba la awali lilivurugika, hivyo kuendeleza pale walipoishia CCM ni kutafuta mkwamo mwingine,” alisema Lissu.
“Lazima wakubali tuanze mchakato huu, kuendeleza kwa maana ya kupiga Kura ya Maoni ni kinyume cha sheria.” Aliongeza kuwa NEC iliwahi kusema Sheria ya Kura ya Maoni haitekelezeki hasa kwenye suala la upigaji wa kura za Wazanzibar na Watanganyika.
Alishauri kuundwa upya kwa Bunge la Katiba ili mchakato huo uanzie alipoishia Jaji Warioba. Kuhusu suala la Mahakama ya Rushwa, ambalo limewekwa kwenye Ilani ya CCM, Dk Mwakyembe alisema mchakato wake unatakiwa kuanza.
“Hili suala la Mahakama maalumu kushughulikia mafisadi na wahujumu uchumi mchakato wake tayari unatakiwa kuanza,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema wakati wa kampeni, Rais John Magufuli alikuwa akilisisitizia sana kwenye mikutano yake, akieleza namna atakavyopambana na mafisadi katika utawala wake. Dk Mwayembe alisema wizara yake ina changamoto nyingi na kwamba kwa sasa anatembelea idara mbalimbali ili kujua utendaji wake kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyezahapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.