MTANZANIA
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekumbwa na kashfa kubwa baada ya watu wawili wanaodaiwa kuwa wahalifu sugu kutoroka katika Kituo cha Polisi Kurasini usiku wa kuamkia juzi.
Watuhumiwa hao, wanadaiwa kushiriki matukio makubwa ya uhalifu ambayo yametikisa nchi katika siku za hivi karibuni.
Taarifa za uhakika kutoka kwenye vyanzo vyake ndani ya jeshi hilo, zinasema watuhumiwa hao walikuwa watatu, lakini waliofanikiwa kutoroka ni wawili.
Chanzo chetu kilisema kuwa mtuhumiwa mmoja alikamatwa wakati akiwa kwenye harakati za kukimbia.
“Kuna wahalifu wawili wametoroka usiku wa kumkia jana (juzi), wanadaiwa kuhusika katika matukio mbalimbali ya kiuhalifu.Hatujui wamekimbilia wapi, nakuhakikishia polisi watawatia mbaroni tu.Sina uhakika, lakini ninavyojua polisi watakuwa wameanza msako mkali,” kilisema chanzo chetu.
Alipotafutwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu ili kutoa ufafanuzi wa tukio hilo, alimtaka mwandishi wetu kuwasiliana na kamanda wa mkoa husika au Kamishina wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
“Sina taarifa ya kuwapo tukio hili, nakuomba uwasiliane na makamanda wahusika au Kamanda Kova watakusaidia,” alisema IGP Mangu.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkodya ili kutoa ufafanuzi wa tukio hilo, alisema hadi jana jioni hakuwa na taarifa hizo, lakini alimtaka mwandishi wa gazeti amtafute Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke kwa ufafanuzi zaidi.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Andrew Satta alipoulizwa kuhusu kutoroka kwa watu hao, alisema hakuna tukio kama hilo.
Alisema huo ni uvumi tu wa watu, pia hakuna operesheni iliyofanyika hivi karibuni ya kuwakusanya watu zaidi ya 30 na kama ni wahalifu sugu wanakaa gerezani na si kituoni.
“Ndugu mwandishi, kwanza unaposema kuwa wahalifu hao walitoroka katika Kituo cha Polisi Kurasini ambacho ni maalumu kwa wahalifu sugu, kwa kweli hatuna kituo kama hicho.
“Hata kama tumefanya operesheni maalumu ya kuwakamata wahalifu katika mikoa yote, hatuwezi kuwaweka idadi kubwa ya wahalifu eneo moja.
Naye Naibu Kamishina wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro, alipoulizwa na gazeti hili kuhusu tukio hilo, alisema yeye hana mamlaka ya kuzungumza kwa sababu mzungumzaji yupo.
MTANZANIA
Mkutano wa kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli juzi uliingia dosari, baada ya watu wawili kufariki dunia na wengine 17 kujeruhiwa.
Tukio hilo la aina yake, lilitokea juzi jioni mkoani Morogoro wakati Dk. Magufuli alipohutubia maelfu ya wananchi wa mkoa huo katika Uwanja wa Jamhuri.
Vifo hivyo ni kutokana na msongamano wa watu kuwa mkubwa wakati wakitoka uwanjani, hali iliyosababisha baadhi yao kupoteza maisha kwa kukosa hewa na wengine kujeruhiwa baada ya kuanguka na kukanyagwa.
Idadi kubwa ya majeruhi hao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro wakiendelea kupata matibabu.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa, Ritha Lyamuya alithibitisha kupokea majeruhi hao.
Dk. Lyamuya alimwambia Rais Kikwete kuwa waliopoteza maisha katika tukio hilo, ni mwanafunzi wa darasa la tano, Ramadhan Abdalah, anayesoma Shule ya Msingi Mkundi na Grace George mkazi wa Kata ya Kilakala.
“Mheshimiwa Rais, katika tukio hili watu wawili wamepoteza maisha na wengine 17 wamejeruhiwa.
“Hii imetokana na msongamano wa watu kuwa mkubwa wakati wanatoka uwanjani… mlango wa kutokea ulikuwa mmoja tu.
“Baadhi ya watu waliishiwa nguvu na kuanguka chini na kujikuta wakikanyagwa na wenzao katika harakati za kutoka uwanjani,”alisema.
Dk. Lyamuya, aliwataja majeruhi waliolazwa kuwa ni Mariana Mkunda, Nasra Abdalha, Christopher Luice, Frola Maduka, Jalia Mohamed na Prodencia Chuma.
Wengine ni Zahela Shanite, Fatuma Omar, Sania said, Sifa Mohemed, Ally Juma, Kokoliko Ramadhan na Awadhi Kenedy.
Hata hivyo, Dk. Lyamuya alisema kati ya hao, majeruhi saba wameruhusiwa na wengine bado wanaendelea na matibabu.
Alisema majeruhi mmoja ambaye hakumtaja jina, hali yake ni mbaya.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alituma salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa walipoteza ndugu zao.
Alisema amesikitishwa na vifo hivyo na kusisitiza kuwa watu waliopoteza maisha walikwenda katika mkutano kwa mapenzi ya chama chao.
“Nimesikitishwa na vifo hivi, marehemu walikwenda kwenye mkutano ule kwa amani na upendo mkubwa wa chama chao…Mungu aziweke roho zao mahali pema,”alisema Rais Kikwete.
“Hakukuwapo na utaratibu wowote wa polisi kulinda usalama wa raia ndani ya uwanja kwa kusimamia utaratibu wa kutoka, badala yake askari wote walikuwa wakitizama na kusimamia zaidi ulinzi wa viongozi wa kitaifa pale uwanjani,”alisema mwananchi mmoja na kuongeza. “baada ya polisi kugundua watu wameanza kuzimia na kupoteza fahamu,walianza kuzunguka huko na kule na kuanza kuokoa waliokuwa wamezidiwa kwa kukanyagwa na wengine ambao walikuwa wamezirai.
MWANANCHI
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu amesema hakuna sheria inayozuia wagombea urais, ubunge na udiwani kufanya kampeni zaidi ya saa 12 jioni isipokuwa ni kanuni za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
GP Mangu alisema hakuna mahali palipoandikwa, lakini kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa na NEC na wadau wake, kinachofuata ni utekelezaji.
IGP Mangu alisema hayo baada ya kuulizwa hatua zinazoweza kuchukuliwa baada ya mgombea wa CCM, Dk John Magufuli kuzidisha muda wa kampeni mjini Morogoro alikotumia dakika zaidi ya 15 juzi.
Pia, wakati uzinduzi wa kampeni zake, Agosti 23 jijini Dar es Salaam, mgombea huyo alizidisha dakika 33. Jana mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa naye alimaliza mkutano wake wa kampeni Mbezi Dar es Salaam saa 12.15.
Mangu alisema kuzidisha muda wa mikutano yao ya hadhara baada ya saa 12.00 jioni ni kuvunja kanuni zilizowekwa na tume ingawa siyo kosa la jinai. “Hakuna sheria inayozuia mkutano kufanyika zaidi ya muda huo. Ni kanuni tu ndizo zinasimamia hilo hivyo ni jukumu la Tume kuchukua hatua.
Kwa askari wangu inakuwa ni changamoto kumlinda mhusika na kama maadui zake watamshambulia,” alisema. Alisema jeshi lake linatumia weledi kusimamia haki na wajibu na kamwe haliwezi kuingilia makubaliano ya watu au taasisi yoyote kama ilivyo kati ya NEC na vyama vya siasa.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alirejea wito wake kwa vyama na wafuasi wake kuzingatia makubaliano yanayosimamia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. “Tunaendelea kuvikumbusha vyama vya siasa kuzingatia kanuni walizojiwekea na kuwaelimisha wafuasi wao juu ya maadili ya uchaguzi.
Alisema, maadili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2015 Sura ya 2.1(c) inaviagiza vyama vyote vya siasa kufanya mikutano ya kampeni kati ya saa 2.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni. Wabanduaji mabango IGP Mangu alisema polisi itawafungulia mashtaka ya kuharibu mali wale wote watakaokamatwa kuhusika na kubandua au kuchana picha za matangazo ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi.
“Kanuni na maadili ya uchaguzi zinazuia wanachama na wafuasi wa chama kimoja kuharibu matangazo au mabango ya kampeni ya mgombea wa chama kingine.
Hivyo yeyote anayefanya hivyo anakiuka maadili waliyoafikiana baina na tume na vyama vya siasa,” alisema Mangu. “Kama atajitokeza mlalamikaji, basi mlalamikiwa atakuwa na kesi ya kujibu juu ya kuharibu mali. Hizo picha ni mali ya mtu au chama fula
MWANANCHI
Aliyekuwa Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Willibrod Slaa amesema anasubiri kwa hamu kujibiwa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kama alivyotangaza kanisani kwake Jumapili iliyopita.
Akiwa kanisani hapo juzi, Askofu Gwajima alikaririwa akisema atajibu mapigo kuhusu tuhuma zilizotolewa dhidi yake na Dk Slaa katika hotuba yake ya Septemba Mosi. Katika hotuba hiyo, Dk Slaa alimwita kiongozi huyo wa Kiroho kuwa ni mshenga wa Edward Lowassa kwa Chadema.
Mwanasiasa huyo mstaafu alizungumza kwenye Hoteli ya Serena baada ya kutoelewana na viongozi wenzake wa Chadema kumpokea Lowassa ajiunge na chama hicho.
“Ukweli unasemwa kama ulivyo, hauyumbishwi yumbishwi, kama anataka kukanusha au kujibu chochote basi afanye hivyo,” alisema Dk Slaa.
Alisema anamshangaa Askofu Gwajima alipohojiwa na gazeti hili baada ya hotuba yake alikanusha kuwa mshenga hali akijua kuwa alizungumza naye (Dk Slaa) wakiwa pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, mke wake, Josephine Mushumbusi na baadhi ya viongozi wa chama hicho.
“Ninachosema kama hana hofu ya Mungu aendelee na akitaka kukanusha au kujibu mapigo ajibu,” alisema.
Hata hivyo, Dk Slaa alikanusha kuwatuhumu maaskofu 30 kati ya 34 kupewa fedha na badala yake alisema alikuwa ananukuu kile alichosema Gwajima katika kikao kilichofanyika Julai 27.
“Askofu Gwajima alisema hayo wakati akinishawishi nimkubali Lowassa nikiwa nyumbani kwangu Julai 28,” alisema Dk Slaa. Pia, alikanusha kumtuhumu Rostam Aziz kutoa kiasi cha Sh15 bilioni kwa ajili ya kampeni badala yake alisema maneno hayo yalitamkwa na Askofu Gwajima mw
MWANANCHI
Mgombea urais wa Chadema anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa amesema hakutakuwa na muda wa kupoteza iwapo atachaguliwa akisema ataanza kushughulikia ahadi zote ikiwamo ya ujenzi wa viwanda kwa ajili ya kutatua tatizo la ajira mara tu baada ya kuapishwa.
Lowassa alisema kila alichoahidi ataanza kukifanyia kazi punde tu baada ya kuapishwa: “Nitajenga viwanda kukabiliana na ajira, ada za shule na mengine ndani ya siku hizo.
“Nikiingia madarakani, hakuna mgeni atakayefanya biashara bila kuingia ubia na wazawa. Lazima tuwajali vijana wetu kwa kuwajengea mazingira wezeshi,” alisema mgombea huyo aliyewasili Bunju saa 9.30 alasiri akitokea Tabora. Ili kufanikisha hayo, aliwataka vijana kulinda kura zao siku ya uchaguzi ili zisiibwe.
Akizungumza katika mkutano wake uliofanyika kwenye Uwanja cha Shule ya Msingi Bunju ‘A’, Lowassa alisema wananchi wana wasiwasi na NEC kwamba haitatenda haki kwa sababu ya ukaribu wake na CCM.
Aliwataka vijana kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kufanya kazi mbili, kwanza kupiga kura na pili ni kulinda kura zao huku akisisitiza kwamba ana uhakika kwamba hataibiwa kura ng’o.
Aliwataka wananchi kufanya uamuzi mgumu kuiondoa CCM madarakani ili wajihakikishie huduma bora za jamii katika serikali ya awamu ya tano.
Alisema zimebaki siku 48 kwa wananchi kuamua hatima ya maisha yao yajayo akiwataka kuwachagua wagombea wa Ukawa ili waondoe msongamano wa magari jijini, kuboresha mfumo wa elimu kuanzisha viwanda vitakavyotengeneza ajira kwa wananchi. Soma zaidi habari hii kupitia Mwananchi EPaper
NIPASHE
Mwanasheria wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando, amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam, huku hali yake ikielezwa kuwa tete baada ya kuugua ghafla juzi nyumbani kwake.
Marando ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema, amelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete hospitalini hapo kwa ajili ya kupata matibabu.
Mmoja wa wauguzi wa zamu katika kitengo hicho ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa madai siyo msemaji wa mgonjwa huyo wala hospitali, alisema Marando alifikishwa hospitalini hapo juzi akiwa na hali mbaya.
Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa watu wa karibu na Marando hali yake inaleta matumaini ikilinganishwa na alivyofikishwa hospitalini hapo juzi.
“Alifikishwa hapa jana usiku (juzi), mimi sikuwapo ila hali yake ilikuwa mbaya lakini kwa mujibu wa ndugu zake amboa ndiyo wako naye hapa wanasema anaendelea vizuri ikilinganishwa na juzi,” alisema.
Alisema kutokana na hali yake kuwa mbaya hawawezi kuruhusu waandishi wa habari kuchukua taarifa yoyote na kwamba hata mke wake amekataa kutoa taarifa za mume wake hadi hapo atakapopona.
“Hata mkienda hamuwezi kuongea naye chochote na tangu asubuhi ukimuuliza kitu anakuangalia tu na anapotaka kuzungumza anabaki anaguna, kwa hiyo kwa hali yake hawezi kuzungumza,” alisema muuguzi huyo.
Alisema wanamatumaini hali ya Marando itakuwa nzuri zaidi baada ya siku mbili kwani kuna dawa wamempatia ambazo zinahitaji apumzike.
“Unajua hawa wanasiasa wanakosa muda wa kupumzika kutokana na kazi zao na hata hapa tunamuona anahamu ya kuzungumza chochote lakini hawezi kutokana na hali yake ndiyo maana tunataka apumzike zaidi,” alisema.
Naye mmoja wa ndugu wa Marando ambaye pia hakutaka kujitambulisha jina lake, alisema mwanasheria huyo aliugua gafla akiwa nyumbani kwake juzi usiku.
“Jana mchana hadi jioni (juzi) nilikuwa naye lakini nilishangaa kupigiwa simu usiku kuelezwa kuwa aliugua ghafla akiwa nyumbani kwake na hata hivyo hatujaweza kuzungumza naye zaidi ya kupewa taarifa za hali yake na mke wake,” alisema ndugu huyo.
Alisema tangu wamempeleka hospitalini hapo bado hali yake ni mbaya ingawa anaendelea na matibabu.
Sababu za ndugu hao kuishia nje zilielezwa kuwa ni kutokana na hali ya Marando kutohitaji usumbufu wa watu kuingia wodini.
Miongoni mwa ndugu waliokuwa hospitalini hapo ni mama mzazi wa Marando ambaye alikuwa amekaa nje akisubiri taarifa ya hali ya mwanaye.
Mtu mwingine wa karibu na Marando ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema, aliugua ghafla akiwa nyumbani kwake na kukimbizwa hospitali ya kwanza ambayo hata hivyo hakutaja jina na baada ya kumpatia huduma ya kwanza walisema hawawezi kumtibu na hivyo kuhamishiwa Hospitali ya Muhimbili.
“Hapa hospitali walimleta usiku akaanza kupatiwa matibabu na hali yake ilikuwa mbaya lakini baada ya kupatiwa matibabu inaendelea vizuri kidogo,” alisema.
Kwa upande wa mke wake ambaye pia hakutaka kujitambulish jina alisema kuwa, hawezi kuzungumzia hali ya mumewe bila ridhaa yake.
Mkewe huyo alitoka wodini majira ya saa 11:00 jioni na kuwapatia ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa wamesimama nje ya jengo hilo taarifa ya hali ya mumewe.
Alisema ni kweli mumewe ni mgonjwa lakini taarifa ugonjwa wake ataitoa mwenyewe.
“Ni kweli mume wangu ni mgonjwa lakini siwezi kumzungumzia bila kibali chake na kuna waandishi wengine wamekuja sijawapa taarifa. Huyu ni mwanasiasa na mnafahamiana, akipona tu atazungumza mwenyewe kila kitu,” alisema na kuondoka eneo hilo.
Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, John Steven, alithibitisha kupokelewa Marando hospitalini hapo juzi saa 4:00 usiku.
“Ni kweli Marando kalazwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete anapata matibabu lakini taarifa kamili ya ugonjwa wake unaweza kuipata kwa mwenyewe wodini au kwa ndugu,” alisema Steven.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, alisema hana taarifa ya kuugua kwa Marando.
NIPASHE
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amewataka watumishi wa Bohari ya Dawa (MSD), kukaa mguu sawa kwa sababu hatakubali kusikia hospitali za serikali zikikosa dawa kama ilivyo sasa.
Dk. Magufuli alisema inashangaza kuona wananchi wanateseka kwa kukosa dawa kwenye hospitali za serikali na wagonjwa kuandikiwa kwenda kununua dawa hizo kwenye mduka binafsi.
Alitoa onyo hilo jana wilayani Kilindi, mkoani Tanga wakati akiwahutubia wananchi kwenye mkutano wa kampeni.
“Hawa wanaohusika na kusambaza madawa wakae mguu sawa maana serikali ya Magufuli haitakubali kuona wananchi wanaendelea kunyanyasika kwa ukosafu wa dawa wakati kwenye maduka binafsi zipo,” alisema Dk. Magufuli na kushangiliwa na wananchi hao.
Magufuli alisema hajaomba nafasi ya urais kufanya majaribio, hivyo watumishi wazembe serikalini wanaokwamisha huduma za maendeleo ya Watanzania wanapaswa kujitazama upya.
Aidha, Dk. Magufuli alisema Tanzania si maskini kwani ina raslimali nyingi isipokuwa mafisadi wachache na wengine wakiwa serikalini ndio wameifikisha nchi pabaya kwa kutumia nafasi zao vibaya.
“Nipeni urais muone namna nitakavyowashughulikia hawa mafisadi, hawa ndiyo wamesababisha wananchi wengine kuichukia serikali kwa kuwa wamekuwa wakitumia fedha zao kuwanyanyasa wananchi wa hali ya chini ambao wanakosa huduma hospitalini,” alisema Dk. Magufuli.
Mgombea huyo alisema nafasi ya urais inamtosha, hivyo wasihangaike na wagombea wa vyama vingine ambao alisema wamekuwa wakitoa ahadi ambazo hawana uwezo wa kuzitekeleza.
“Nafasi ya urais inanitosha kwa sababu lengo langu ni kuwatumikia Watanzania, najua hapa Songe mnahitaji lami, nimeweza kujenga kilomita nyingi nchini na madaraja mengi, siwezi kushindwa kilomita tano za lami hapa Songe,” alisema.
Katika hatua nyingine, msafara wa Dk. Magufuli uliingia mkoani Tanga kutoka Morogoro kwa kishindo kutokana na mapokezi makubwa aliyoyapata kutoka kwa wanachama wa CCM na wananchi wa mkoa huo.
Msafara wa mgombea huyo ambao ulikuwa ukitokea mkoani Morogoro, ulisimama katika vituo zaidi ya 14 ukiwa njiani kuelekea wilaya ya Kilindi na Handeni mkoani humo ambapo alikuwa akizungumza na wananchi waliokuwa wamefurika barabarani wakimsubiri.
Dk. Magufuli alilazimika kusimama njiani na kuzungumza na wananchi hao na kuwanadi wagombea wa udiwani wa maeneo husika kutoka CCM ambao walikuwa barabarani na wananchi wakimsubiri kwa muda mrefu.
Mgombea huyo alielezea kufurahishwa na mapokezi hayo ya aina yake aliyopata mkoani humo na kuahidi kuwa ameondoka na deni na njia pekee ya kuwalipa wananchi hao ni kuhakikisha anatatua kero zao.
NIPASHE
Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), limeingia lawamani kutokana na usumbufu na hasara kubwa wanayowasababishia watumiaji wa nishati hiyo kufuatia tangazo lao la ‘ghafla’ kuwa sehemu kubwa ya nchi itakuwa gizani kuanzia jana.
Tanesco ilitoa tangazo hilo kwa kile ilichokieleza kuwa ni kutaka kuanza kujaribu mitambo ya kufua umeme wa gesi iliyopo Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), Dk. Samwel Nyantahe, ameitupia lawama Tanesco kutokana na kuitangazia nchi kuingia ‘gizani’ kwa wiki nzima kuanzia jana pasipo kutoa taarifa mapema ili wananchi wajiandae kukabiliaana na hali hiyo.
Akizungumza na Nipashe jana, Dk. Nyantahe, alisema kabla ya Tanesco kufikia hatua hiyo ilipaswa kutoa ‘notsi’ hata ya wiki moja ili watu wajiandae.
“Sisi wenyewe tumeshtuka kusikia kwamba kutakuwa na shida ya umeme wiki nzima, ninashindwa kufahamu ni jambo gani ambalo Tanesco hawakujua mpaka wanatoa taarifa za ghafla za kukatika kwa umeme wiki nzima pasipo kuwaandaa watu waweke mambo yao sawa,” alihoji Dk. Nyantahe.
Aliongeza: “ Wangetoa notsi, ingekuwa rahisi watu kujiandaa kwa kuweka vitu vyao sawa, kama ni wenye kutafuta majenereta watafute ili mambo mengine yaendelee hasa kwa wafanyabiashara.”
Alisema Tanesco kufanya hivyo, kunarudisha nyuma uzalishaji na kwamba kama ulikuwa unapanda ni lazima utashuka na huku ukichangia kuongezeka kwa gharama za uzalishaji.
“Hii ni kuyumbisha uzalishaji kwa nchi, yaani unapoanza kupanda, unaporomoka tena kutokana na sababu ambazo zingeweza kuzuilika,” alisema.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini, Johnson Minja, alisema Tanesco kukatakata umeme kutawaathiri kwa kiwango kikubwa kwa kuwa shughuli zao zinaendeshwa kwa kutegemea nishati hiyo.
Alisema wiki nzima ni kubwa kwa wafanyabiashara, hivyo kuna baadhi ya mambo yatasimama kwa muda.
Mbali na hilo, pia alisema gharama za uzalishaji zitaongezeka na kwamba ni lazima walaji nao wataumia kwa sababu bidhaa zitapanda.
Kwa mujibu wa Mramba, mikoa itakayoathirika ni yote inayopata umeme wa Gridi ya Taifa ukiwamo Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Dodoma, Morogoro, Singida, Mwanza, Mara, Mbeya, Iringa, Tabora, Shinyanga, Manyara na Zanzibar.
NIPASHE
Wakati kampeni za uchaguzi mkuu zikishika kasi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeanza kupokea baadhi ya vifaa vya kupigia kura huku karatasi zikitarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi huu.
Kwa kujibu wa Nec, vifaa vilivyoanza kuingia nchini ni vile masanduku, taa, fulana na fomu wakati karatasi za kupigia kura zikitarajiwa kupokelewa kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 15, mwaka huu kutoka Afrika Kusini.
Kaimu Mkurugenzi wa Ununuzi na Menejimenti ya Lojistiki wa Nec, Eliud Njaila, aliliambia Nipashe kuwa karatasi hizo zitapokelewa kwa awamu na kusambazwa katika maeneo husika.
Njaila alisema ifikapofika Septemba 29, mwaka huu Nec itapokea karatasi za kupigia kura za mikoa ya kanda ya ziwa na kanda ya kati zinazoindwa na mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga, Kigoma, Dodoma, Singida na Tabora.
Alisema ifikapo Oktoba 5 hadi 6, mwaka huu, Nec itapokea karatasi za kupigia kura kwa mikoa ya nyanda za juu kusini na mikoa ya kusini zinazoundwa na mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa, Rukwa, Ruvuma, Mtwara na Lindi.
Alisema baada ya kupokea vifaa vya mikoa hiyo, pia watapokea karatasi kwa ajili ya mikoa ya kanda ya Pwani na kanda ya Kaskazini zinazoundwa na mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara na kueleza kuwa vitakapowasili Nec itavisambaza vifaa hivyo moja kwa moja katika maeneo husika.
“Ndege haiwezi kuvibeba vifaa vyote, ndiyo maaana vitakuja kwa awamu, vikifika tu tunavipokea na kuvipeleka mikoani,” alisema Njaila.
Alisema idadi ya karatasi wanazotarajia kuzipokea zitalingana na idadi ya wananchi waliojiandikisha ambao ni milioni 24.
Aidha, Njaila aliwataka Watanzania kujiandaa kupiga kura itakapofika Oktoba 25, mwaka huu kwa kuwa kila kitu kinakwenda vizuri.
Wiki iliyopita, Nec kupitia kwa Mjaila, ilieleza kuwa gharama za awali kwa ajili ya vifaa vya kura kwa ajili ya uchaguzi huo zimefikia Sh. bilioni 31.25.
Alieleza kuwa kati ya gharama hizo, Dola za Marekani 6, 145, 882.92 (Sh. bilioni 13.1) zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya karatasi za kura.
Hata hivyo, gharama za vifaa hivyo ni tofauti na zile zilizotumiwa na tume hiyo kwa ajili ya kununulia mashine 8,000 za Biometric Voters Registration (BVR) na shughuli nzima ya uandikishaji kwenye daftari hilo nchi nzima ambazo kwa mujibu wa Nec, ni Sh bilioni 133.
HABARILEO
Watoto wawili wa f a m i l i a moja wilayani hapa, wamekufa maji baada ya mtumbwi waliokuwa wakitumia kuvulia samaki, kugonga mwamba na kuzama katika Ziwa Victoria.
Akithibitisha tukio hilo la juzi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alisema siku ya tukio, majira ya saa moja jioni watoto hao waliiba mtumbwi na kuingia nao Ziwa Victoria eneo la kisiwa cha Bumbile kwa lengo la kuvua samaki.
Alifafanua kwamba wakati wakiendelea na uvuvi, ghafla mtumbwi wao uligonga mwamba na kusababisha watoto hao kuzama na kufa maji.
Aliwataja watoto hao kuwa ni Andisius Masenene aliyekuwa anasoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Bumbile na mdogo wake, Rugumisa Masenene aliyekuwa anasoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi ya Bumbile. Kamanda alisema umri wao haujafahamika.
Kwa mujibu wa Mtendaji wa Kata ya Bumbile, Herman Mgango, mwili wa Andisius ulipatikana na kwamba mwili mwingine unaendelea kutafutwa.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos