MWANANCHI
Baadhi ya watu jana mchana ‘waligida’ pombe za bure baada ya Fuso lililokuwa limebeba masanduku ya bia kupinduka katika Barabara ya Mandela, Dar es Salaam baada ya Fuso hilo kugongwa kwa nyuma na lori na kupinduka.
Kundi hilo la vijana hao wakiwemo madereva wa bodaboda walivamia na kuchukua chupa za bia na kunywa huku wengine wakinywa mfululizo.
Tukio hilo lilidumu kwa takribani 20 kabla ya polisi kuongeza nguvu.
Vijana wengine waliingia mitaroni ambako bia ziliangukia na kuzichukua bila kujali kuwa zimepasuka, muda mfupi baadae wengine wakaanza kulewa.
Dereva wa Fuso hilo Mohamed Said alisema mzigo huo wa bia aliutoa katika Kiwanda cha Serengeti kwenda Kituo cha Polisi Mkoa wa Pwani.
“Hizi bia zilikuwa katika masanduku 500 ni mali ya Polisi Pwani, ajali hii ni uzembe unaoonekana wazi kuwa wa dereva wa lori, hata polisi wakija kupima watajua nani mwenye kosa,” alisema Said kabla ya Fuso lingine kufika na kuchukua bia hizo na kuondoka nazo.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori aliyekuwa akitokea njia ya pembeni kuingia barabara kuu bila tahadhari japo dereva wa lori amekataa kusababisha ajali hiyo.
MWANANCHI
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewajibu wabunge waliokosoa kitendo cha mawaziri watano waliotajwa kwenye kashfa za Operesheni Tokomeza na ESCROW akisema Ikulu haikuhusika kuwasafisha bali ilitangaza matokeo ya uchunguzi wa tume na kwa sasa uchunguzi wao unafanywa na TAKUKURU.
Waliotangazwa kusafishwa ni Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Shamsi Vuai Nahodha (Mambo ya Ndani), Balozi Hamisi Kagasheki (Maliasili na Utalii) na David Mathayo, aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Mifugo ambao walishinikizwa na Bunge kujiuzulu baada ya kuhusishwa na kashfa mbalimbali.
Mwingine ni Prof. Sospeter Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliackim Maswi ambao walisimamishwa wakati wa sakata la ESCROW.
“Taarifa ya kwanza iliyomhusu Maswi na ilitokana na kazi iliyokuwa imefanywa na timu ya makatibu wakuu baada ya Tume ya Maadili kuwa imemaliza kazi yake. Taarifa ya pili ilikuwa inahusiana na Operesheni Tokomeza,” alisema Pinda.
Katika maelezo ya Balozi Sefue kuhusu Profesa Muhongo na Maswi, alisema waziri huyo wa zamani wa nishati na madini alionekana hana hatia na ndiyo maana hakupelekwa mbele ya Kamati ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ambayo pia ilimchunguza Maswi na kumuona kuwa hakuhusika katika uchotwaji huo wa fedha wala kupata mgawo.
“Tume ilisema wengine walioona kuwa wana kesi ya kujibu wanaendelea nao (kuwahoji) mpaka mwisho. Na wakaniambia katika suala hili vyombo vingine (Takukuru na polisi) vinafanya uchunguzi wa kitaalamu na vikipata ushahidi hakutakuwa na pingamizi hata kama Tume imetoa uamuzi wake,”—Waziri Mkuu Pinda.
Waziri Mkuu Pinda amesema TAKUKURU wanaendelea na uchunguzi wao na muda ukifika watatoa uamuzi wao na kama itaonekana kuna ushahidi mzito wahusika wote watafikishwa mahakamani.
“Taarifa ya Ikulu haikulenga kumsafisha mtu. Ile ilikuwa ni taarifa kwa umma juu ya kazi ya uchunguzi kuhusu operesheni hiyo.”—Waziri Mizengo Pinda.
JAMBO LEO
Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu amesema kauliz zilizotolewa na Mbunge Joshua Nassari ni za kutapatapa na zimejaa uzushi na ukosefu wa busara.
Nyalandu amesema kitendo cha Mbunge kusimama Bungeni na kutoa kashfa badala ya kueleza masuala ya kisera au kiutendaji ni kupungukiwa busara na jamii haina budi kumpuuza.
Juzi Mbunge Joshua Nassari alisema Nyalandu kazi yake kubgwa ni kuzunguka katika mapori ya akiba na kupiga picha na mbwa wa kizungu na kupokea helikopta za msaada.
Nyalandu alisema kauli hiyo iliyotolewa Bungeni na Nassari ni ya kichonganishi kati ya Serikali na wananchi japo haiwezi kuikatisha tamaa Serikali kwa sababu ni suala la kawaida kwa wapinzani..
NIPASHE
Licha ya serikali kutochukua hatua kuokoa maisha ya raia wake, mtoto wa mwanasheria mmoja wa Dar es Salaam, amenusurika kifo kutokana na kutumia dawa zinazotolewa kliniki za raia wa Korea Kaskazini.
Kliniki hizo zilizopo maeneo ya Temeke, Magomeni na Kariakoo zimedaiwa kwa muda mrefu kutoa dawa za asili zisizokuwa na majina au maelekezo kuhusu namna ya kuzitumia.
Bernadeta Shayo ambaye ni mwanasheria alisema mtoto wake, Gabriel Shayo alitumia dawa alizopewa kwenye kliniki hizo wakati akisumbuliwa na matatizo ya kifua ambapo baada ya kupata dawa hizo alipata maumivu makali, kubanwa kifua na kutapika damu.
Bernadeta amesema alipofikishwa hospitalini hapo, Gabriel alibainika kushambuliwa na vijidudu kifuani na tiba yake iligharimu Sh. 150,000, na kiasi kingine cha Sh.10,000 kila siku kwa muda wa wiki mbili bila kupewa risiti.
Bernadeta alisema baada ya muda huo, hali ya Gabriel ilizidi kuwa mbaya huku akipata maumivu makali kifuani, waliporudi tena Hospitali walimwambia kwamba vijidudu havijaisha na kutaka malipo ya Sh. 150,000 kwa ajili ya matibabu ya wiki mbili za nyongeza.
Baadae Gabriel alipata tiba kwenye hospitali ya serikali hadi Februari mwaka huu ambapo hali yake inaendelea vizuri.
Waandishi wa gazeti la NIPASHE walifika kwenye kliniki hiyo na baada ya kujitambulisha walimzuia asiingie ndani na kusema hakuna mtu wa kutoa ufafanunuzi juu ya suala hilo.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Richard Kayombo, alisema kitendo cha hospitali hizo kutoa huduma bila kutoa risiti ni kuvunja sheria na utaratibu wa haraka unafanyika kuzifanyia uchunguzi.
NIPASHE
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amesema licha ya muda wa vikao vya Bunge kubadilika na kutumia saa nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali, wabunge hawatalipwa posho ya ziada.
“Mabadiliko ya ratiba hayana uhusiano na mabadiliko ya posho. Wabunge hawalipwi malipo ya ziada ‘over time’ wala hawalipwi kwa saa”—Mwigulu Nchemba.
Aliongeza kuwa posho za kujikimu na vikao zimebakia kama zilivyokuwa hapo awali ambako, walikuwa wanaanza kikao saa 3:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana na kurejea tena saa 11 jioni hadi saa 1:45 usiku.
Wabunge wanaelezwa kusaini Sh. 150,000 kila siku ikiwa ni posho ya kujikimu ya Sh. 80,000 na 70,000 kwa ajili ya vikao ambapo kiasi hicho ni tofauti na posho za madereva, mafuta pamoja na gharama nyingine ambazo wanalipiwa na serikali.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.