Paul Pogba amefungiwa kutojihusisha na soka kwa miaka minne kwa kosa la kutumia dawa za kusisimua misuli.
Kiungo huyo wa kati wa Ufaransa na Juventus alisimamishwa kwa muda mwezi Septemba baada ya kukutwa na testosterone. Pogba alishinda Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa mwaka 2018, miaka miwili baada ya kuwa mwanasoka ghali zaidi duniani wakati Manchester United ilipomsajili kwa rekodi ya £89m.
Pogba, ambaye atafikisha umri wa miaka 31 mwezi Machi, alikuwa mchezaji wa akiba ambaye hajatumika Juventus katika mchezo wa Serie A dhidi ya Udinese tarehe 20 Agosti alipopimwa na kukutwa na testosterone – dawa iliyopigwa marufuku.
Shirika la kitaifa la kupambana na dawa za kusisimua misuli la Italia lilimsimamisha kazi Pogba na ombi kutoka kwa mwendesha mashtaka wa michezo wa Italia kumpa Pogba marufuku ya miaka minne, adhabu ya juu zaidi inayopatikana kwao, ilikubaliwa.
Pogba sasa anatarajiwa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wao katika mahakama ya juu zaidi ya michezo, Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo, nchini Uswizi, lakini kufungiwa kwa miaka minne kunaweza kukasababisha mwisho wa maisha yake katika ngazi ya juu.