Nyota wa Manchester United Robin Van Persie amekiri kuwa huenda akaihama klabu hiyo pale ambapo mkataba wake utakapomalizika ndani ya kipindi cha miezi 18 ijayo .
Robin Van Persie ametoa kauli hii baada ya kujikuta akicheza chini ya kiwango kwa muda mrefu sasa ambapo ameshindwa kuonyesha ubora wake aliowahi kuwa nao kipindi alipohamia toka Arsenal .
Van Persie amekuwa kwenye wakati mgumu kiasi cha kumfanya kocha wa klabu hiyo Louis Van Gaal kufikiria kumuacha nje ya kikosi cha kwanza na kutoa nafasi kwa wachezaji wengine wa nafasi ya ushambuliaji .
Kiwango cha mdachi huyu hata hivyo kimeonekana kuanza kurejea kati hali yake ya kawaida katika michezo ya hivi karibuni ambapo ameweza kuifungia United mabao 8 tu , idadi ambayo si nzuri kwa mshambuliaji wa kiwango cha Van Persie .
RVP kama ambavyo mashabiki hupenda kumuita aliisaidia United kutwaa ubingwa katika msimu wake wa kwanza akifunga mabao 26 kwenye ligi kuu ya England ukiwa msimu wake wa kwanza baada ya kuuzwa toka Arsenal kwa ada ya uhamisho ya paundi milioni 24 .
Van Persie mwenyewe amekiri kuwa hajawa kwenye kiwango chake bora na kwamba anapaswa kuongeza bidii ili kuisaidia timu yake.
Hadi sasa United inashika nafasi ya 4 nyuma ya Southampton kwenye ligi kuu ya England huku wakiwa na kumbukumbu ya kumaliza kwenye nafasi ya 7 kwa msimu uliopita wakiwa chini ya David Moyes.