Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Jokate Mwegelo amewahimiza Wanafunzi kusoma kwa bidii kutokana na kuwekewa mazingira mazuri ya kujifunza na kufundishia ambapo amesema namna pekee ya Wanafunzi kuonesha shukrani kwa Serikali na Wafadhili wanaopeleka msaada Shuleni ni kusoma kwa bidii na kuendelea kufanya vizuri katika masomo yao.
Jokate amesema hayo katika hafla ya kukabidhi kompyuta 25 katika Shule ya Sekondari ya Semkiwa Wilayani Korogwe Mkoani Tanga, Shule hiyo pamoja na Shule ya Sekondari Kwaluguru ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni zimekabidhiwa Kompyuta 25 kila moja na Shirika la Camara Education Tanzania.
Shirika hilo limetoa msaada wa kompyuta 100 zenye thamani ya Sh. Milioni 37 kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambayo ina jukumu la kisheria la kukusanya michango kwa ajili ya sekta ya elimu nchini, kompyuta hizo 100 zimetolewa kwa Shule nne za Sekondari zilizoko kwenye Mikoa ya Tanga na Pwani ambapo, kila shule imepata kompyuta 25 kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kupata masomo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Afisa Miradi wa Camara Education Tanzania, Bi. Asia Bonanga amesema shirika la Camara Education Tanzania linajikita katika kupeleka teknolojia ya mawasiliano mashuleni ili kusaidia jitihada za kupatikana kwa elimu bora nchini.