Watoto takribani 200 wa kiume na wa kike wameadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika leo June 16,2023 kwa kuungana na Wadau wa kutetea haki za Watoto katika matembezi ya amani yaliyoanzia Hospitali ya Agha Khan na kuishia Viwanja vya Farasi, Dar es salaam lengo likiwa ni kupaza sauti kupinga ukatili kwa Watoto na kupinga muendelezo wa ucheleweshaji wa mabadiliko ya vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa vinavyomruhusu Mtoto wa kike kuolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18.
Wadau hao wanasema mabadiliko ya vifungu hivi viwili vya Sheria ya Ndoa yamecheleweshwa kwasababu ni miaka minne imepita sasa tangu mwaka 2019 ambapo Mahakama ya Rufaa ilitamka bayana kupitia kesi ya Rebeca Gyumi kwamba vifungu hivi ndani ya sheria vinavunja Katiba kwa kukiuka haki ya usawa na ulinzi kwa Watoto.
Katika maadhimisho ya mwaka huu Watoto hao wameungana na Mashirika nane yakiwemo Msichana initiative, Flaviana Matata Foundation, Tai Tanzania, Missing Child, Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni na Jamii Forums.
Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka ifikapo June 16 kwa lengo la kuwakumbuka Watoto waliouawa na Serikali ya kibaguzi Soweto mwaka 1976 wakiwa katika maandamano ya kudai haki zao.