Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amepokea vifaa vyenye thamani ya Tsh. Milioni 190 kutoka kwa Taasisi ya Doris Mollel katika Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni vifaa tiba kwa ajili ya watoto njiti, Madawati 450 pamoja na mitungi ya gesi 300 kwa ajili ya Mama wajawazito na wahudumu wa Afya.
Katika hafla hiyo, Makamu wa Rais ametoa rai kwa wadau mbalimbali nchini wakiwemo wanamuziki, wachezaji na hata waigizaji kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti).
Ameipongeza Taasisi ya Doris Mollel ambayo imekuwa ikitekeleza shughuli zake kwa takriban miaka nane sasa katika kusaidia Serikali kutoa huduma kwa watoto waliozaliwa kabla ya wakati na pia kusaidia katika utoaji wa vifaa tiba vinavyotumika kuokoa maisha ya watoto hao.
Aidha, amekemea tabia za ukatili hususani kuwapiga wanawake wajawazito kwani madhara yake ni makubwa katika kupatikana kwa mtoto. Ametoa rai kwa viongozi wa dini, Serikali na kisiasa kushirikiana katika kuwachukulia hatua wale wote wanaofanya ukatili kwa wanawake wajawazito.
Dkt. Mpango ameipongeza taasisi ya Doris Mollel kwa kushirikiana na Oryx Energies Tanzania kujikita katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa akina mama wajawazito kwa kuwa tafiti zinaonesha mama mjamzito anayetumia nishati chafu katika kipindi cha ujauzito anakuwa yuko hatarini kupata mtoto njiti.
Amesema mpango huo ni muhimu kuwa endelevu kwani utatusaidia katika suala zima la kudhibiti uharibifu wa mazingira, ambao huchangiwa kwa kukata miti hovyo kwa ajili ya matumizi ya nishati.
Ametoa rai kwa Wananchi wa Buhigwe na maeneo mbalimbali nchini kuungana kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Pia Makamu wa Rais amewapongeza mchezaji wa kimataifa Mbwana Samatta (@samagoal) na Mwanamuziki wa kizazi kipya Ali Saleh Kiba maarufu kama Ali Kiba (@alikiba) kwa kuhamasisha kuhusu changamoto wanazopitia watoto njiti nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Taasisi ya Doris Mollel, Bi Doris Mollel amesema Taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na serikali katika jitihada za kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati pamoja na changamoto zinazopelekea kuzaliwa kwa watoto hao. Pia amesema taasisi hiyo imeshiriki katika kutoa vifaa tiba hapa nchini pamoja na utungaji sera za kukabiliana na ongezeko la watoto wanaozaliwa kabla ya wakati katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa.
Bi. Mollel ameongeza kwamba taasisi imeendelea na jitihada za kuhakikisha marekebisho ya sheria ya likizo yanafanyika ili kuwapa muda wa miezi sita wakina mama wanaojifungua watoto kabla ya wakati kutokana na changamoto zinazowakumba. Pia amesema tayari taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wamefanikiwa kuhakikisha bima binafsi zinatoa huduma kwa mtoto anayezaliwa kabla ya wakati kupitia gharama ya bima ya mama wa mtoto.