Ushahidi mpya wa mpango wa puto wa “kijasusi” wa China ikiwa ni pamoja na safari za ndege juu ya Japan na Taiwan umefichuliwa, ripoti za vyombo vya habari zilisema.
Japan imethibitisha kuwa puto zimeruka katika eneo lake na kusema iko tayari kuziangusha katika siku zijazo, BBC iliripoti.
Uhusiano kati ya Marekani na China ulitumbukia katika msukosuko mapema mwaka huu, wakati puto linalodaiwa kuwa la kijasusi la China lilipotunguliwa kwenye pwani ya Marekani.
China ilidai puto lililoonekana kaskazini-magharibi mwa Marekani mwishoni mwa Januari lilikuwa meli ya kiraia, iliyotumika kwa utafiti wa kisayansi kama vile hali ya hewa na kwamba lilikuwa tukio lisilotarajiwa na la pekee.
Mchambuzi wa zamani wa Asia Mashariki wa CIA Corey Jaskolski,aliiambia shirika la habari la BBC kuwa alipata ushahidi wa puto moja kuvuka kaskazini mwa Japani mapema Septemba 2021. Picha hizi hazikuchapishwa hapo awali.
Jaskolski pia anaamini ushahidi unaonyesha kuwa puto hili lilizinduliwa kutoka ndani kabisa ya China, kusini mwa Mongolia, BBC iliripoti.
Japan ni mshirika wa karibu wa Marekani na majeshi mengi ya Marekani yamewekwa huko kuliko katika nchi nyingine yoyote ya kigeni.