Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Mwinyi amezindua rasmi kituo cha usafirishaji cha Kampuni ya Silent Ocean kwenye Mji wa Foshan huko China kitakachokuwa na kazi kubwa ya upokeaji na usimamizi wa mizigo inayosafirishwa kutoka China kuja Tanzania.
Katika hotoba yake kwenye ufunguzi, Mkurugenzi Mtendaji wa SILENT OCEAN Salaah S. Mohamed amesema kituo hiki kipya na cha kisasa kitaiwezesha Kampuni hiyo kupokea na kuhifadhi idadi kubwa ya makontena kutoka idadi ya sasa ya makontena 600 na kufikia makontena 1000 kwa mwezi.
“Kituo hiki kipya kitarahisisha utekelezaji wa maelewano yaliyofikiwa na Viongozi wetu wawili wa Kitaifa Mh. Rais Samia Suluhu Hassan na Rais XI Jinping wa China wa kupanua ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Tanzania na China” ——— Salaah S. Mohamed.
Ukiachia Rais Dr. Mwinyi na Mkewe Mama Mariam, Viongozi waliohudhuria uzinduzi huu ni Waziri wa Viwanda na Biashara Dr. Ashatu Kijaji, Balozi wa Tanzania Nchini China Mbelwa Kairuki na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Mambo ya Nje ya Guangdong Luo Jun.
Silent Ocean ( @silent_ocean_ltd ) ni Kampuni maarufu na iliyoshinda Tuzo nyingi za ubora kwenye usafirishaji mizigo kwa miaka 19 sasa ambapo imekua ikisafirisha mizigo kuileta Tanzania ikitokea China, Dubai, Marekani, Uturuki na India.