Wafanyabiashara walioathiriwa na maporomoko ya tope,mawe na magogo kutoka mlima Hanang mkoani Manyara na kupelekea kuharibu bidhaa zao wamepatiwa malipo ya fidia ya Bima yenye thamani ya Zaidi ya shilingi Milioni 260 ilitolewa na benki ya NMB ili kuwafidia hasara waliyoipata na kuwawezesha kuendelea na Biashara zao.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya hundi hiyo ya fidia Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini Baraka Ladislaus amesema fedha hizo ni sehemu ya fidia kwa waliokata Bima kwenye Biashara na Bima za Mikopo Kupitia Bank ya NMB, huku akisema Bank hiyo itaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kufahamu umuhimu wa Bima.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Bima benki ya NMB Martin Masawe amesema Benki hiyo imekuwa ikitoa Bima kwa Wananchi wa Kada zote kuanzia Bima ya Shilingi elfu kumi kwa Mwaka Mzima ili kuwawezesha kujikinga na majanga pindi yanapotokea, na Mfano Mzuri ni kwa Machinga wa jijini Mwanza na Wafanyabiashara wa Hanang waliokumbwa na Maafa hayo.
Nae Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Bima nchini Dokta Baghayo Saqware amesema ulipaji wa fidia hiyo ni utekelezaji wa matakwa,kanuni na taratibu za kisheria huku akipongeza benki ya NMB kwa kutekeleza utaratibu huo Kwa wakati.
Mkuu wa wilaya ya Hanang Janeth Mayanja ameiomba benki ya NMB kuendelea kuwafikia Wafanyabiashara na wajasiriamali wadogowadogo ili kuwasaidia kupata elimu juu ya faida za za Bima lakini pia wananchi kuachana na mikopo yenye masharti kandamizi ili kuwainua kiuchumi.