Leo Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana amezindua semina ya mikopo ya wasanii inayoratibiwa na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania na kutolewa na Benki ya CRDB. Semina hiyo iliyowahusisha zaidi ya wasanii 400 kutoka mikoa 12 nchini ilifanyika makao makuu ya Benki ya CRDB.
Waziri Chana alisindikizwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania ambaye ni Mkurugenzi wetu Mtendaji, Abdulmajid Nsekela pamoja na Afisa Mtendaji wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, Nyakaho Mahemba na kupokelewa na Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki yetu, Boma Raballa.
Kuanzia leo, wasanii wote nchini kuanzia wa muziki, maigizo, uchongaji na uchoraji na fani nyingine zinazohusiana na utamaduni na sanaa wataweza kupata mkopo nafuu wa kuendeleza mawazo au miradi waliyonayo ili kuikuza zaidi.
Kwa makubaliano yaliyopo kati ya Mfuko na Benki, sasa wasanii wanaweza kukopeshwa mpaka Shilingi milioni 100 watakazozirejesha mpaka kwa miezi 24.