Ni wiki ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la kujenga Taifa JKT ambapo jeshi hilo limeendelea na shughuli mbalimbali ikiwemo kurudisha kwa jamii na katika kushirikiana na jamii jeshi hilo limefanya usafi katika kituo cha Afya Halmashauri ya wilaya ya Chamwino pamoja na kutoa zawadi kwa wakina mama waliojifungua.
Mkurugenzi wa Ustawi wa Jamii wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT Kanali Regina Matina amesema katika mwendelezo wa shughuli zinazofanywa na Jeshi hilo kuelekea miaka 60 ya jeshi hilo liamua kushiriki shughuli za kijamii kwasababu jeshi hilo ni sehemu ya jamii.
“Tumeamua kutembelea hospitalini hapa kufanya usafi na kutoa zawadi katika wodi ya wazazi kwani JKT ni sehemu ya jamii tumeungana na wazazi kama ilivyo majukumu ya JKT ni malezi ya vijana ,uzalishaji mali na ulinzi,na hawa ndiyo wazazi wanaotupatia vijana ,tukaona ni muhimu tusimalize maadhimisho haya bila kuwaona wazazi.”Kanali Regina Matina
Hata hivyo Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo John Daniel amelishukuru Jeshi la Kujenga Taifa kwa kuchagua kituo hicho kuwa sehemu ya eneo lilitumika katika kuadhimisha miaka ya miaka 60 ya jeshi hilo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1963.
“JKT tumekuwa tukishirikiana nao mara nyingi,tumekuwa tukiwaomba msaada mbaimbali na wanatusaidia tunaomba waendelee na moyo huo wa kusaidia jamii.” John Daniel Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Chamwino.