Polisi nchini India walitumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya maelfu ya waandamanaji waliokuwa wakidai kujiuzulu kwa kiongozi mkuu wa mashariki mwa nchi hiyo, wakimtuhumu kwa kushindwa kusimamia uchunguzi wa ubakaji na mauaji ya daktari wa hospitali mapema mwezi huu.
Waandamanaji hao walikuwa wakilalamikia mauaji ya daktari mwenye umri wa miaka 31 aliyekuwa kazini katika Hospitali ya R.G. Kar Medical College, Kolkata. Tukio hilo limechochea hasira na maandamano ya kitaifa, huku waandamanaji wakisisitiza mazingira salama kwa wafanyakazi wa afya katika hospitali za India.
Maelfu ya madaktari na wahudumu wa afya wamegoma nchi nzima wakidai usalama zaidi mahali pa kazi, huku maandamano hayo yakionekana kuathiri huduma za afya kwa wagonjwa.
Waandamanaji walijaribu kuvunja vizuizi vya polisi na kuandamana hadi ofisi ya Mamta Banerjee, kiongozi wa jimbo la Bengal magharibi. Wakituhumu ukosefu wa usalama kwa wanawake, waandamanaji wameonyesha kukasirishwa na ongezeko la vurugu dhidi ya wanawake nchini humo, licha ya sheria kali zilizowekwa baada ya tukio la ubakaji wa mwanafunzi mnamo 2012.
Familia ya daktari aliyeuawa imedai tukio hilo lilihusisha ubakaji wa kundi, na polisi wamekamata mshukiwa mmoja.