Polisi wa Colombia wanatanya msako katika milima kaskazini mwa nchi hiyo kumtafuta baba wa mshambuliaji wa Liverpool Luis Diaz aliyetekwa nyara.
Mamake Diaz ameokolewa lakini mamlaka ya Colombia imeongeza kasi ya kumtafuta baba yake, huku mchezaji huyo akiwa amerejea nyumbani kuwa na wanafamilia.
Polisi wamekuwa wakifanya doria za angani katika safu ya milima ya Perija, ambayo inapita mpaka na Venezuela na kufunikwa na msitu.
Katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii, mkurugenzi mkuu wa polisi wa Colombia William Salamanca alionyeshwa akitembelea operesheni hiyo ili “kuwatambua makomandoo wetu kwa ushujaa na kujitolea kwao kumwokoa akiwa salama”.
Polisi wametoa zawadi yenye thamani ya karibu £39,000 kwa taarifa zitakazosaidia kumuokoa Luis Manuel Diaz.
Siku ya Jumatatu, Salamanca alihimiza tahadhari kuhusu ripoti kwamba Luis Manuel anaweza kuwa tayari amepelekwa Venezuela, akiashiria ugumu wa kuvuka milima ya Perija.
FIFA na Shirikisho la Soka la Colombia wametoa msaada kwa Diaz, 26, huku Liverpool ikiruhusu mchezaji huyo kurejea nyumbani.