Polisi wa Ujerumani wamekanusha madai kwamba waliwashauri mashabiki waliokuwa wakisafiri kwenda nchini humo kwa ajili ya michuano ya Euro 2024 kutumia bangi badala ya pombe, baada ya ripoti za habari kuibuka zikisema kinyume chake.
Polisi nchini Ujerumani wamekanusha madai kuwa walipendekeza mashabiki wa soka wavute bangi badala ya kunywa pombe wakati wakizuru nchini humo kutazama michuano ya kandanda ya Euro 2024.
Kanusho hilo limekuja baada ya jarida la Uingereza la The Sun kuripoti siku ya Ijumaa kwamba msemaji wa polisi wa Ujerumani Stephan Knipp alisema kuwa “haina shida kwa mashabiki kuvuta bangi mitaani”.
“Ikiwa tutaona kikundi cha watu wakinywa pombe na wanaonekana kuwa na fujo, na kikundi kingine kinavuta bangi, bila shaka tutaangalia kikundi hicho kinakunywa pombe,” Knipp aliripotiwa kusema.
Hata hivyo, polisi wa Gelsenkirchen wamekanusha madai hayo, wakiandika ripoti ya Sun kuwa ni “uongo”.
Polisi “watahakikisha usalama wa mashabiki wakati wa Mashindano ya Kandanda ya Ulaya na watakabiliana na vikundi vikali vinavyofanya fujo, bila kujali vileo,” kulingana na chombo cha habari cha Ujerumani The Local.de.
“Hatuwahimiza mashabiki wa soka kuvuta bangi,” msemaji huyo aliripotiwa kuongeza.