Polisi wameliondoa genge linalodaiwa kutumia huduma ya teknolojia iliyosaidia wahalifu kutumia jumbe za ulaghai kuiba kutoka kwa waathiriwa nchi mbalimbali.
Wamekamata watu 37 kote ulimwenguni na wanawasiliana na wahasiriwa.
Maafisa wanasema vijana ambao walikua na mtandao ndio walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuangukia kwenye kashfa ya “hadaa”.
Teknolojia hiyo iliwaruhusu walaghai wasio na ujuzi wa kiufundi kuwashambulia waathiriwa kwa jumbe zilizoundwa ili kuwahadaa wafanye malipo mtandaoni.
Polisi walilenga tovuti ya genge hilo, LabHost, ambayo ilisaidia wahalifu kutuma jumbe hizo na kuwaelekeza waathiriwa kwenye tovuti ghushi zinazoonekana kuwa malipo halali ya mtandaoni au huduma za ununuzi.
Ilikuwa imewawezesha wahalifu kuiba taarifa za utambulisho, ikiwa ni pamoja na nambari za kadi 480,000 na Pin codes 64,000, zinazojulikana kwa lugha ya jinai kama “fullz data”, polisi walisema.
Wapelelezi hawajui ni pesa ngapi zilizoibiwa lakini wanakadiria tovuti ya LabHost ilipata faida ya karibu £1m ($1.25m).