Mshukiwa amekamatwa katika kile polisi wamekiita kuwapiga risasi wanafunzi watatu wa chuo wenye asili ya Kipalestina katika jimbo la Vermont nchini Marekani.
Polisi katika mji wa Burlington walimkamata mshukiwa mwenye umri wa miaka 48, aliyetambuliwa kama Jason J Eaton, Jumapili mchana, kulingana na ripoti za habari za Marekani.
Wahasiriwa watatu, Hisham Awartani, Kinnan Abdalhamid na Tahseen Ahmed, walipigwa risasi Jumamosi jioni karibu na chuo kikuu cha Vermont. Wanafunzi hao, wanaosoma vyuo vikuu tofauti nchini Marekani, wamesalia hospitalini wakiwa na majeraha ya risasi.
Wanafunzi hao, wawili kati yao ni raia wa Marekani na wa tatu mkazi halali, walikuwa wakitembelea Burlington kusherehekea sikukuu ya Shukrani na familia.
Huku maelezo zaidi ya shambulio hilo yakiibuka, polisi wanasema wanachunguza ufyatuaji huo kama uhalifu wa chuki.
“Katika wakati huu wa kushtakiwa, hakuna mtu anayeweza kutazama tukio hili na asishuku kuwa huenda lilikuwa uhalifu unaochochewa na chuki,” Mkuu wa Polisi wa Burlington Jon Murad alisema katika taarifa.
“Kwamba kuna dalili kwamba ufyatuaji risasi huu ungeweza kuchochewa na chuki ni wa kutisha, na uwezekano huu unapewa kipaumbele” na polisi, Meya Miro Weinberger alisema.