Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa, ugonjwa wa kisukari unaathiri idadi kubwa ya watu barani Afrika kutokana na ukuaji wa haraka wa miji, mtindo mbovu wa maisha kama wa kukaa chini sana, utaratibu mbovu wa kula chakula pamoja na unywaji wa pombe na ulevi.
Shirika hilo lilitoa taarifa yake hiyo jana Jumanne ambayo ilikuwa ni Siku ya Kisukari Duniani. Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, alisema, bara hilo lina watu wazima milioni 24 wanaoishi na kisukari, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi milioni 55 ifikapo mwaka 2045.
Amesema, ugonjwa wa kisukari ulisababisha vifo vya watu 416,000 barani Afrika mwaka 2021 na inakadiriwa kwamba utakuwa moja ya sababu kuu za vifo barani Afrika ifikapo mwaka 2030, kama jamii za watu wa bara hilo hawatobadilisha mtindo wao wa maisha.