Rais wa Jamhuri ya Rwanda Paul Kagame leo January 14, 2018 amefanya ziara ya kikazi ya siku moja nchini kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli.
Kagame amewasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere na kupokelewa na Rais Magufuli na viongozi wengine mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, baada ya kutoka Airport walielekea Ikulu ambapo walifanya mazungumzo faragha na baadae walizungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari.
President JPM amesema wamekubaliana kuanza ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) kati ya Isaka Tanzania na Kigali Rwanda yenye urefu wa kilometa 400 uanze mwaka huu 2018 na wamewataka Mawaziri wa Miundombinu kukutana ndani ya kipindi cha wiki mbili kuanzia sasa ili kuweka mipango ya utekelezaji.
JPM amebainisha kuwa kumekuwa na ongezeko la mizigo ya Rwanda inayosafirishwa kupitia Tanzania iliyofikia tani 950,000 kwa mwaka lakinki biashara kati ya nchi hizi mbili sio ya kuridhisha, hivyo wamekubaliana kuboresha zaidi mazingira ya biashara ikiwemo kuimarisha miundombinu ya reli na barabara.
“Tukijenga reli kutoka Isaka hadi Kigali, na sisi huku tunajenga kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na tukaunganisha Dodoma hadi Isaka, mizigo mingi ya Rwanda itasafirishwa kupitia bandari ya DSM, biashara itakua zaidi na ajira zitaongezeka,”– President JPM
“Kule Lulenge Ngara, Burundi na Rwanda kote kuna madini ya Nickel, tukijenga miundombinu yetu tutasafirisha madini haya na tutaongeza biashara. Na reli hii itatumiwa na nchi nyingine za Burundi, DRC na Uganda, kwa hiyo ni jambo muhimu sana kwa uchumi wetu na majirani.”- President JPM
Rais Magufuli amemhakikishia Kagame kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano na Rwanda kwa manufaa ya wananchi na ipo tayari kumuunga mkono atakapochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) katika kikao cha wakuu wa nchi na Serikali kinachotarajiwa kufanyika mwishoni mwa January, 2018 Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
“Rais Kagame nakupongeza sana, unafanya kazi kubwa ya kuwapigania wananchi wako, Watanzania tunajua ulikoitoa Rwanda na tunajua ulipoifikisha, nakuhakikishia tutaendelea kushirikiana katika jukumu la kuwaletea wananchi maendeleo” – President JPM
Nae President Kagame amemshukuru Rais Magufuli kwa mwaliko wake na amempongeza kwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi yake na Tanzania.
President Kagame amesema yeye Rais Magufuli wameamua kufanya kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo na ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili mipango yote waliyojiwekea itekelezwe ikiwemo kuinua biashara na kuongeza ajira, na pia ameshukuru kwa kuwa tayari kumuunga mkono atakapochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa AU.
President Kagame amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku moja hapa nchini na amerejea nchini kwake Rwanda.
HD VIDEO: MIPANGO YA KAGAME KWA VIJANA WA AFRIKA AKIWA MWENYEKITI WA AU