Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -Mipango na Maendeleo, Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo, leo tarehe 01 Novemba 2024 amewasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/26 lakini pamoja na mambo mengine Prof. Kitila Mkumbo ameeleza mafanikio kadhaa yaliyopatikana kufuatia uamuzi wa serikali wa kuikabidhi Kampuni ya DP World kuendesha sehemu ya Bandari ya Dar es Salaam.
Kampuni ya DPW imekwishawekeza TZS 214.425 bilioni sawa na 31% ya TZS bilioni 675 zinazopaswa kuwekezwa katika kipindi cha miaka [5] kwa ajili ya manunuzi ya mitambo ya kisasa; ukarabati wa mitambo iliyokuwa ya TPA; na usanifu na usimikaji wa mfumo wa TEHAMA wa kisasa wa uendeshaji wa Bandari
Kuongezeka kwa shehena zinazohudumiwa kutoka shehena 141,889 mwezi Mei 2024 hadi kufikia shehena 168,336 mwezi Septemba 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.6 katika kipindi cha miezi mitano
Pia amesema kuwa katika kipindi cha miezi mitano gharama za matumizi ya uendeshaji wa bandari zimepungua hadi kufikia asilimia 2.7 ya makusanyo wakati ambapo matumizi yalikuwa yanaongezeka kwa asilimia 15.1 kwa mwezi kabla ya kukabidhiwa uendeshaji wa bandari kwa kampuni na Serikali imeshakusanya jumla ya shilingi bilioni 325.3 ikiwa ni mapato yanayotokana na shughuli za mikataba iliyoingiwa kati ya TPA na DP World.
Aidha, Prof. Mkumbo ameeleza mafanikio ya kiuchumi na kijamii yanayotokana na kukamilika kwa ujenzi wa Reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ikiwemo kutoa ajira zaidi ya 30,176 za moja kwa moja na ajira zaidi ya 150,000 zisizo za moja kwa moja,ajira hizi zimetengeneza pato la TZS bilioni 358.74.
Kupungua kwa muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma kutoka wastani wa masaa kumi kwa basi hadi masaa matatu na nusu kwa Treni pamoja na kupunguza ajali na kuokoa maisha ya watu.
Akiongea leo November 01,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/2026 Prof. Kitila Mkumbo amesema faida nyingine ni pamoja na kutunza mazingira/kupungua kwa uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa kuwa usafiri wa treni unatumia nishati ya umeme na kwa kuwa safari za mabasi zimepungua imekuwa kichocheo cha shughuli za utalii katika ukanda ambao reli inayopita, hususan Hifadhi ya Mikumi na Hifadhi ya Ruaha (kupitia Stesheni ya Kilosa)