Waziri wa Nchi , Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako kwa kushirikiana na Oryx Gas wamegawa mitungi 600 ya Oryx na majiko yake kwa vikundi vya wanawake wilayani Kasulu kwa ajili ya kuwawezesha kutumia nishati safi ya kupikia ambayo ni rafiki kwa mazingira.
Aidha kutolewa kwa mitungi hiyo kwa vikundi vya wanawake hao kunalenga kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye anahimiza wananchi kutumia nishati safi ya kupikia ili kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mitungi hiyo ya gesi ya Oryx 600 yakiwa na majiko yake kwa wanawake hao wa Wilaya ya Kasulu Waziri Ndalichako ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini amesema mitungi hiyo inakwenda kuleta auheni kwa makundi ya wanawake kwani wataachana na matumizi ya kuni na mkaa na kutumia nishati safi ya kupikia ambayo ni gesi ya Oryx.
“Kugawa mitungi hii kwa wananchi wetu ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono juhudi za Rais Dk .Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akihamasisha utunzaji wa mazingira kwa kutoharibu misitu yetu kwa kukata miti kwa ajili ya kupata kuni na mkaa.Hivyo niendelee kuwaomba wananchi tutunze mazingira.”
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas Tanzania Araman Benoite amesema mipango ya kampuni yao kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia inakwenda na mpango wa Serikali wa miaka 10 wa matumizi salama ya nishati safi ya kupikia.
Amesema kampuni inatambua kuwa kundi la akina mama ambao kila siku wanahudumia chakula cha Watanzania wengi, wameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi ya kuni na mkaa hivyo, kampuni ya Oryx Gas kwa kushirikiana na Waziri Ndalichako wameamua kuiunga mkono jumuiya hii ikiwa ni hamasa kwa wengine.
Benoite amesema Rais Dk.Samia ameweka lengo la Watanzania kutumia nishati safi, ikiwa ni pamoja na LPG, kuwa angalau asilimia 80 ya watu wote ifikapo mwaka 2032. Kampuni ya Oryx Gas Tanzania inajivunia kuunga mkono maono yake katika kutoa nishati safi ya kupikia.