Rais wa Urusi Vladimir Putin ametoa kile alichokiita “uungaji mkono kamili” kwa Afrika, ikiwa ni pamoja na katika mapambano dhidi ya ugaidi na itikadi kali.
Hotuba hiyo ilisomwa katika mkutano wa kilele katika eneo la mapumziko la Bahari Nyeusi huko Sochi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov kwa viongozi wenzake wa Afrika.
Serikali kadhaa za Kiafrika zimekata uhusiano na washirika wa jadi wa Magharibi na wanatafuta msaada kwa Moscow katika kukabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara ya wanajihadi.
Wakati wa mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso, Karamoko Jean-Marie Traoré alisema Urusi ilikuwa mshirika wa kimataifa anayefaa zaidi kuliko mkoloni wa zamani, Ufaransa.
Ni maoni yaliyotolewa na makoloni kadhaa ya zamani ya Ufaransa na yalitolewa tena na Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop, ambaye alitofautisha ushirikiano wa “dhati” wa Kremlin na uhusiano wa “ukoloni mamboleo” wa madola ya Magharibi.
Alisema pamoja na ushirikiano wa kijeshi, Mali inachunguza miradi mingine ya pamoja katika sekta ya nishati, mawasiliano, teknolojia na madini.
“Kampuni za Urusi zinafanya kazi katika maeneo yote haya na serikali ya Mali na washirika binafsi nchini Mali ili kutoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili watu wa Mali. Pande hizo mbili zimekubaliana kuongeza kasi ili kuhakikisha matokeo ya haraka,” alisema.
Wapiganaji mamluki wa Wagner – ambao sasa wamebadilishwa jina chini ya bendera ya Africa Corps na wizara ya ulinzi ya Urusi, walikuwa chaguo bora kwa viongozi wa kijeshi ambao waliamuru wanajeshi wa Ufaransa na UN kuondoka.
Usaidizi wa Urusi, mara nyingi badala ya kupata malighafi, pia unakuja na ahadi kwamba hakutakuwa na kuingilia mambo ya ndani ya nchi au mafunzo ya jinsi ya kuendesha uchaguzi.