Rais Vladmir Putin alisema siku ya Alhamisi kwamba Urusi imefanikiwa kufanyia majaribio kombora jipya la kimkakati lenye nguvu na imekataa kuondoa uwezekano wa kufanya majaribio ya silaha yanayohusisha milipuko ya nyuklia kwa mara ya kwanza katika zaidi ya miongo mitatu.
Putin alisema kwa mara ya kwanza kwamba Moscow imefanyia majaribio Burevestnik, kombora la nyuklia lenye uwezo wa kusafiri kwa maelfu ya maili.
Pia aliuambia mkutano wa kila mwaka wa wachambuzi na waandishi wa habari kwamba Urusi ilikuwa karibu kukamilisha kazi ya mfumo wake wa makombora ya balestiki ya Sarmat, kipengele kingine muhimu cha kizazi kipya cha silaha za nyuklia.
Putin, ambaye amekumbusha mara kwa mara ulimwengu juu ya uwezo wa nyuklia wa Urusi tangu kuzindua uvamizi wake nchini Ukraine mnamo Februari 24, 2022, alisema hakuna mtu mwenye akili timamu ambaye angetumia silaha za nyuklia dhidi ya Urusi.