Rais wa Urusi Vladimir Putin aliishukuru Korea Kaskazini kwa kuunga mkono hatua yake nchini Ukraine na kusema nchi zao zitashirikiana kwa karibu kushinda vikwazo vinavyoongozwa na Marekani alipokuwa akielekea Pyongyang siku ya Jumanne kwa mkutano wa kilele na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.
Maoni ya Putin yalionekana katika kipande cha picha kilichotolewa na vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini saa chache kabla ya kuwasili kwake kwa ziara ya siku mbili huku nchi hizo zikizidisha mshikamano wao katika kukabiliana na mizozo tofauti na Washington.
Katika mji mkuu wa Korea Kaskazini wa Pyongyang, mitaa ilipambwa kwa picha za Putin na bendera za Urusi. Bango lililotundikwa kwenye jengo lilisema: “Tunamkaribisha kwa uchangamfu Rais wa Shirikisho la Urusi.”
Putin, ambaye atakuwa anafanya safari yake ya kwanza nchini Korea Kaskazini baada ya miaka 24, alisema anashukuru sana uungaji mkono wake thabiti wa hatua yake ya kijeshi nchini Ukraine.
Alisema nchi hizo zitaendelea “kupinga kwa uthabiti” kile alichokitaja kuwa matarajio ya Magharibi “kuzuia kuanzishwa kwa utaratibu wa ulimwengu wa pande nyingi unaozingatia haki, kuheshimiana kwa uhuru, kuzingatia masilahi ya kila mmoja.”
Putin pia alisema Urusi na Korea Kaskazini zitatengeneza mifumo ya biashara na malipo “ambayo haidhibitiwi na nchi za Magharibi” na kupinga kwa pamoja vikwazo dhidi ya nchi hizo, ambavyo alivitaja kuwa “vizuizi haramu na vya upande mmoja.”