Rais wa Russia amesema kuwa Moscow iko tayari kumaliza vita na Kiev kwa amani, lakini hakuna dalili kwamba Ukraine inataka amani.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tass, Rais wa Russia, Vladimir Putin, amesema katika kipindi cha televisheni kwamba Moscow iko tayari kuzungumza na Kiev ili kumaliza mzozo na Ukraine na kuongeza kuwa, kama si uingiliaji kati wa nchi za Magharibi katika vita vya Ukraine vita hivyo vingemalizika miezi 18 iliyopita, lakini Kiev haikutaka jambo kama hilo.
Mnamo Februari 21, 2022, Rais wa Russia alitambua rasmi uhuru wa Jamhuri za Watu wa Donetsk na Luhansk katika mkoa wa Donbas, akikosoa mwenendo wa nchi za Magharibi wa kutotilia maanani wasiwasi wa usalama wa Moscow.
Siku tatu baadaye (Februari 24, 2022), Vladimir Putin alianzisha operesheni maalumu ya kijeshi dhidi ya Ukraine.
Vita nchini Ukraine, pamoja na matokeo yake makubwa ya kisiasa, kijeshi, kiuchumi, kijamii na hata kitamaduni, viko katika mwezi wake wa 24, na nchi za Magharibi bado zinatuma misaada ya silaha kwa serikali ya Kiev.