Leo July 25, 2018 Kamishna Jenerali mpya wa Jeshi la Magereza, Phaustine Martin Kasike amefanya mabadiliko kwa Wakuu wa Magereza wa Mikoa na Vituo vingine vya Magereza nchini, lengo likiwa ni kufanya maboresho ya kiutendaji.
Katika taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano Magereza na Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Lucas Mboje imetaja mabadiliko hayo ambapo aliyekuwa Mkuu wa Magereza Dodoma, Naibu Kamishna wa Magereza(DCP), Julius Sang’udi amehamishiwa Makao Makuu ya Magereza kuwa Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Wafungwa na nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza(SACP), Salum Hussein.
Aliyekuwa Mkuu wa Gereza Mtego wa Simba, Kamishna Msaidizi wa Magereza(ACP), Msepwa Omary amehamishiwa Magereza Mkoa wa Singida kuwa Kaimu Mkuu wa Magereza mkoa huo na nafasi yake inakaimiwa na Mrakibu wa Magereza, Muta Tibalinda.
“Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, Naibu Kamishna wa Magereza (DCP), John Masunga amehamishiwa Makao Makuu ya Magereza kuwa Mkuu wa Kitengo cha Viwanda vya Jeshi la Magereza na nafasi yake imekaimishwa kwa aliyekuwa Mnadhimu wa Magereza Mkoani Tanga, Kamishna Msaidizi wa Magereza(ACP), Emmanuel Lwinga”
Wengine ni aliyekuwa Boharia Mkuu wa Magereza, Naibu Kamishna wa Magereza (DCP), Afwilile Mwakijungu amehamishiwa Makao Makuu ya Magereza kuwa Mdhibiti Mkuu wa Shirika la Magereza na nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi wa Magereza(ACP), Goleha Masunzu.