India imesema inatathmini njia zote za kisheria baada ya mahakama nchini Qatar kuwahukumu kifo maafisa wanane wa zamani wa jeshi la majini la India kwa mashtaka ambayo hayakujulikana.
Ripoti zinasema watu hao waliokuwa wakifanya kazi na kampuni ya kibinafsi nchini Qatar, walikamatwa mwaka jana kwa tuhuma za ujasusi.
Qatar na India hazijafichua mashtaka mahususi dhidi yao.
Siku ya Alhamisi, serikali ya India ilisema “ilishtushwa sana” na itachukua uamuzi huo na mamlaka ya Qatar.
Wizara ya mambo ya nje ya India ilisema katika taarifa yake kwamba inasubiri hukumu ya kamili na kuongeza kuwa inaweka “umuhimu mkubwa kwa kesi hii”.
“Tunawasiliana na familia na timu ya wanasheria, na tunachunguza njia zote za kisheria,” wizara ilisema, na kuongeza kuwa haitatoa maoni zaidi hivi sasa kwa sababu ya “asili ya siri ya kesi hii”.
Taarifa hiyo inawaelezea watu hao kama wafanyikazi wa kampuni ya kibinafsi iitwayo Al Dahra, lakini wameripotiwa kuwa wafanyikazi wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la India.
Mwaka jana, waziri wa mambo ya nje S Jaishankar aliwataja bungeni kama “watumishi wa zamani” wa nchi hiyo.