Raia mmoja wa Libya anayeshukiwa kuunda bomu lililouwa Watu 270 baada ya kuilipua ndege ya Shirika la Pan Am nchini Scotland mwaka 1988 amekamatwa nchini Marekani.
Waendesha mashitaka wa Scotland wamesema Familia za wale waliouawa kwenye mkasa huo zimefahamishwa kwamba Abu Agila Muhammad al-Marimi sasa yuko kizuizini.
Awali alikuwa anashikiliwa nchini Libya akishukiwa kushiriki kwenye mashambulizi dhidi ya klabu moja ya usiku mjini Berlin mwaka 1986.
Wizara ya Sheria ya Marekani imethibitisha kumshikilia Mshukiwa huyo, ikisema kuwa anatazamiwa kufikishwa Mahakamani hivi karibuni mjini Washington, DC.
Al-Marimi ni Afisa wa tatu wa ujasusi wa Libya kufikishwa Mahakamani nchini Marekani kwa mashambulizi dhidi ya ndege hiyo ya shirika la Pan Am iliyokuwa ikiruka kutoka London kwenda New York tarehe 21 Disemba 1988.
Ndege hiyo, Boeing 747, ililipuka ikiwa juu ya Mji mdogo wa Lockerbie, Scotland, na kuwaua Watu 259 waliokuwemo ndani ya ndege na wengine 11 ambao walikuwa mahala ilipoangukia.