Raia wengi wa Nigeria wameghadhabika baada ya ndege mpya kununuliwa kwa ajili ya Rais Bola Tinubu wakati ambapo uchumi unakumbwa na mzozo mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kizazi.
Ndege hiyo imenunuliwa wiki mbili baada ya maelfu ya watu kumiminika barabarani kote nchini kulalamikia njaa inayoongezeka na kupanda kwa gharama ya maisha.
Bw Tinubu ambaye alichaguliwa mwaka jana kuongoza nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika, ameanzisha mageuzi kadhaa ya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta, ambayo imechangia mfumuko mkubwa wa bei, ambao kwa sasa ni zaidi ya 30%.
Rais Tinubu alisema mageuzi hayo ni muhimu ili kupunguza matumizi ya serikali na kuchochea ukuaji wa muda mrefu.
Mnamo Januari, rais wa Nigeria alitangaza kupunguza kwa asilimia 60 ya idadi ya maafisa wa serikali wanaosafiri nje ya nchi , ikiwa ni pamoja na wasaidizi wake mwenyewe.
Hata hivyo Jumatatu, rais aliondoka kuelekea Ufaransa kwa kutumia ndege mpya aina ya Airbus A330, ambayo imekuwa nyongeza ya hivi punde zaidi ya ndege zaidi ya tano za rais.
Gharama ya ndege hiyo haijawekwa wazi, na wala sababu ya safari yake haijaelezwa wazi.